Tafuta DHWTangazaTuandikie
ASET kuingia kwenye ushindani-Asha

Kampuni ya African Stars Entertaiment Tanzania (ASET), imeamua kuingia katika ushindani wa soko la muziki nchini, katika mfumo wa kuwa na bendi itakayoundwa na raia kutoka Kongo.



Naye Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Asha Baraka alisema kampuni yake imefikia hatua hiyo, baada ya kuona hali ya soko la muziki nchini imebadilika na pia kuondoa dhana kwamba hawapendi wanamuziki kutoka Kongo.

Asha alisema bendi ya African Revolution (Twanga Chipolopolo), ndio itakayotengwa kwa ajili ya wanamuziki wa kigeni, ambapo baadhi ya wanamuziki wake wataongeza nguvu kwenye bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta'.

Alisema yeye kama mwanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), anatekeleza ilani ya chama chake ya kutoa ajira kwa kila Mtanzania,lakini watu wamekuwa wakimtafsiri vibaya kwamba hawapendi Wakongo.

Mkurugenzi huyo aliomba aeleweke kwamba yeye ndiye aliyewaleta akina Nyoshi Elsaadat, Rodger Muzungu, Elistone Engai kwa mara ya kwanza hapa nchini wakati huo mkurugenzi huyo akiwa na bendi ya MK Sound.

Alisema akiwa mwanasiasa bado ataendelea kutoa ajira kwa Watanzania, ambapo bendi ya Twanga Pepeta itaendelea kuimarishwa zaidi, ili iweze kutoa ushindani wa hali ya juu.

Asha alisema wiki ijayo anatarajia kutangaza wanamuziki watakaoiunda upya bendi ya African Revolution, ambayo itakuwa na sura tofauti.

Katika hatua nyingine alimalizia kwa kusema kwamba bendi ya African Stars Ijumaa itatumbuiza Lindi, Jumamosi Mtwara na Jumapili itamalizia Masasi.




 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki  Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved.Design by Infocomtechnologies Limited.