Wasanii mnafungwaje luku!
Hata miezi miwili haijaisha tangu kumalizika kwa Mwaka wa Shetani na kuingia kwa mwaka mpya wa 2008 lakini tayari wasanii kadhaa wa Bongo fleva, wenye majina na wasio na majina, wameshaingia kwenye malumbano yasiyo na kichwa wala miguu baina yao.
Kuna wasanii walioingia kwenye `bifu` baada ya upande mmoja kutukanwa kupitia redio.
Kuna wasanii walioingia kwenye bifu baada ya upande mmoja kuanika matatizo ya upande wa pili redioni. Kuna wasanii walioingia kwenye `bifu` baada ya kituo kimoja cha redio kurusha madai ya upande mmoja kuwa WAZO la wimbo fulani ulioimbwa pia na fulani ni MALI ya msanii fulani.
Na wasanii wenyewe wakawa radhi kujibizana kupitia redio hizo, kwa kupingana na kuapizana.
Na katika namna ya ajabu, ni kama baadhi ya wasanii hao wa Bongo fleva wamefungwa luku ya akili na baadhi ya vituo hivyo vya redio vya FM.
Ni kama baadhi ya wasanii wamefungwa luku ya akili bila kujali kiwango cha elimu yao kwasababu, kwamfano, lipo `bifu` ambalo lilizuka baada ya msanii mmoja kuulizwa maoni yake juu ya mtazamo uliodaiwa kutolewa na msanii mwingine katika gazeti.
Katika hali ya kawaida,lilikuwa ni jukumu la msanii aliyedhani hakutendewa haki kuhakikisha kuwa ni kweli hakutendewa haki na msanii mwenzake kama anavyodhani kabla ya kukurupuka na kutoa kashfa dhidi ya mwenzake kupitia mazungumzo ya redio.
Lakini wapi. Kwasababu msanii anayedhani hakutendewa haki yuko kwenye kipaza sauti kinachomfanya asikike kwa maelfu ya mashabiki wake kwa mara moja, akatema sumu kabla ya kujiridhisha kuwa ni kweli amedhalilishwa.
Wasanii wa Bongo fleva ni lazima wafahamu kuwa katika ulimwengu wa sasa wa ushindani mkubwa wa kibiashara miongoni mwa vyombo vya habari, vipo ambavyo vina wafanyakazi ambao wapo tayari kuweka maneno vinywani mwa wahojiwa mara nyingine hata bila kuzungumza na mhojiwa mdaiwa.
Katika hali kama hii ni rahisi kwa wasanii na wapenzi wa Bongo fleva kwa ujumla kumlaumu msanii anayedhani hakutendewa haki au mwenye kutuhumiwa kutomtendea mwenzake haki kwa kuanzisha `bifu` katika kipindi kinachofuatia kumalizika kwa Mwaka wa Shetani.
Lakini katika hali kama hii wa kulaumiwa ni wapiga muziki redioni a.k.a watangazaji kwa kuanzisha `bifu` katika kipindi kinachofuatia kumalizika kwa Mwaka wa Shetani.
Ni wazi,lisingekuwepo `bifu` kati ya wasanii wengi walio katika `bifu` sasa, kwa mfano, kama baadhi ya wapiga muziki wa Bongo fleva redioni wasingekuwa makini katika kupitia kwa nia ya kutafuta chokochoko kurasa za magazeti ya udaku na majigambo ya kawaida ya majukwaa ya muziki wa Hip hop ili kupata mada za vipindi vinavyofuatia vya redio za FM.
Hivyo badala ya wasanii kukurupuka kichwa kichwa kufanya mahojiano yenye kujibu ama kuibua shutuma dhidi ya msanii mwingine wa Bongo fleva, naona ni vizuri akamuuliza Dj wa Radio hiyo ni nini hasa dhamira ya mahojiano hayo.
Muziki wa kizazi kipya ni wa kizazi kipya, lakini jukumu la kwanza la kuuenzi muziki wa Bongo fleva linaangukia kwanza kwa wasanii wenyewe. Hilo ni lazima lifahamike.
Jukumu la kwanza la kuuenzi muziki wa kizazi kipya linaangukia kwa wasanii wenyewe kwasababu naamini wengi kati yao, wakiwemo hata wale waliofungwa luku za akili na wapiga muziki redioni, wanachukulia muziki kuwa ni ajira.
Ni wasanii ndiyo wenye kudai kuendesha ma-Baloon kwa pesa inayotokana na Bongo fleva.
Ni wasanii ndiyo wenye kudai kuporomosha vi-appartment kwa pesa inayotokana na Bongo fleva. Ni wasanii ndiyo wenye kushindana kuwa na mademu wa Ki-bongo kwa pesa inayotokana na Bongo fleva.
Kama mpiga muziki wa Bongo fleva redioni atafaidika moja kwa moja na pesa inayotokana na muziki wa kizazi kipya, basi si kiasi kikubwa sana juu ya dau la juu zaidi la vocha ya simu. Na pengine ndiyo sababu `watangazaji` wetu hawaoni hasara ya kuchonganisha Ma-Mc.
Ma-Mc wakumbuke umaarufu wa msanii hutokana na ubora wa kazi zake. Si ujuzi wa kuchokoza ma-`bifu` redioni, si ujuzi wa kujibu `live` redioni mapigo ya kashfa zinazodaiwa kutolewa dhidi yao.
Chunguza, kabla Mc hujajikuta umechokoza. Liwe somo la kwanza la leo.
Lakini pia mezea, kabla Mc hujajikuta umezalisha `bifu`. Liwe somo la pili la leo.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala