Uzinduzi wa Haleluya kufanyika Machi 23
Ile albamu mpya wa muziki wa injili Haleluya Collections Volume 4 imepangwa kuzinduliwa ndani ya tamasha la Pasaka, litakalofanyika Machi 23 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions Alex Msama, alisema kwamba uzinduzi wa albamu hiyo utakwenda sambamba na burudani mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Msama alisema maandalizi ya tamasha hilo la kuabudu na kumshukuru Mungu kwa njia ya muziki wa Injili yanaendelea vema.
Alisema wanatarajia kuwa na wasanii mahiri wa hapa nyumbani na nje katika tamasha hilo, na maandalizi yote yamekamilika na wanawaomba wadau wajitokeze ili wawaunge mkono.
Alisema watu mbalimbali hawana budi kubadilika katika maisha ya sasa, kwani wengi wameegemea kusherehekea katika mambo yasiyompendeza Mungu na kwamba sasa ni wakati wa kusherehekea kwa muziki wa Injili.
Mkurugenzi huyo alisema tamasha hilo litaambatana na matukio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa tuzo kwa watu wanaosaidia jamii na wasanii wa muziki huo kwa kutoa msaada kwa jamii.
Nyimbo zilizo ndani ya albamu hiyo na wasanii wake ni 'Wa Milele' (Angela Chibalonza aliyeimba kabla hajafariki dunia), Adui Yako (Flora Mbasha), Usifiwe (Ency Mwalusaka) na Kwanini? (Rose Muhando).
Nyingine ni pamoja na Yupo Njiani (Modest Morgan), Kutembea na Yesu (Catherine Mchepa), Yohana (Kijitonyama Custom Sound), Msamaria (Hosana Group) na Ninapenda Kuishi (Amos Muungwana).

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala