Tafuta DHWTangazaTuandikie
Hiphop si Business!

Nimepokea mawazo yenye kina kutoka kwa msomaji wetu mmoja ambaye anajadili utafiti wa Madee kuwa `Hip Hop Haiuzi` na mapokeo ya wasanii wa fani hiyo juu ya utafiti huo.

Anaeleza:
Mwanamuziki wa hip hop Madee ameibua mjadala juu ya muziki anaoufanya wa kufokafoka kutokana na wimbo wake wa `Hip Hop Haiuzi`. Anasema aina hiyo ya muziki kwa sasa haina faida kibiashara kulinganisha na Bongofleva iliyo katika mahadhi kama zouk, R&B...

Baadhi ya wanamuziki wanapinga hoja hiyo bila kujibu hoja yenyewe kutokana na kuudhiwa na mashairi ya Madee toka kundi la Tip Top Connection lenye nyota wengine wakiwemo wanaofanya vizuri sokoni kama Z.Anto na zamani MB Doggy.



Wengi wa Wana-hip hop asilia wanaelewa kuwa muziki huo ni tiba kwao hivyo madai ya Madee ni ya kuangaliwa kwa usasa na ni ya kupuuzwa kiasili ya muziki wenyewe.

Lakini hoja ya Madee si ya kupuuzwa moja kwa moja kwani muziki wa kizazi kipya umewawezesha baadhi ya wanamuziki kuwa na maisha yanayoridhisha.

Hivyo Madee anastahili kupongezwa kutokana na kunena kwa utashi wake anavyoona mwelekeo wa biashara ya muziki wa Bongofleva, hususan mwelekeo mbaya wa miondoko hiyo ya hip hop. Jambo la msingi ni kutazama hoja yake na asili ya muziki wenyewe na mustakabali wa Bongofleva na wanamuziki au waumini wa hip hop kwa ujumla wake.

Kwa mtazamo wa ki-hip hop huwezi kuzungumzia asili ya muziki huo na asilimia 100 za biashara bali ukombozi kutokana na ukandamizaji wa aina mbalimbali unaofanyika katika jamii.

Hoja ya Madee juu ya biashara ya faida katika hip hop bila shaka imetokana na kuvutiwa na mafanikio ya chipukizi Z.Anto ambaye hafanyi muziki wa hip hop kama alivyo yeye.

Amevutiwa na mafanikio ya Z.Anto kwa kuwa wengi wa wanamuziki wa bongo fleva wanadhani mafanikio ni kumiliki magari au vito vya thamani kubwa kama vinavyomilikiwa na baadhi ya wanaoimba zouk au R&B ambavyo anaona haviwezi kumilikiwa na wanaofanya hip hop.

Kwa kifupi, mtazamo wa Madee kuwa magari ni mambo muhimu katika shughuli za kimuziki ili kupima uwezo wa biashara ya aina ya muziki fulani, ni kosa la kiupembuzi kibiashara kwani huwezi kutathmini faida ya duka la jirani kwa kuhesabu idadi ya wateja wanakuwepo eneo hilo.

Muziki kibiashara siyo albamu moja au wimbo mmoja pekee bali wigo mpana wa kujenga msingi wa kibiashara. Hivyo kuulilia muziki wa hip hop kwamba hauuzi ni kwenda kinyume na asili ya muziki huo ambao nia ya waanzilishi ilikuwa kujikomboa kutokana na ubaya waliotendewa na tabaka la juu katika jamii, ingawa nakubali itageuka kuwa biashara nzuri iwapo tu wanamuziki watatunza asili yake.

Mabadiliko ya utamaduni ndiyo yanachangia historia kuwa na maana mbalimbali kulingana na muda au wakati husika.

Hivyo tafsiri ya baadhi ya mambo ikiwemo muziki wa hip hop hupata maana ambayo awali haikuwepo kama Madee anavyotutaka tukubaliane naye kwa mujibu wa utafiti wake.

Yapo mambo mawili makuu yanayochangia kubadilika kwa utamaduni wa muziki wa hip hop ambayo ni usasa na Umagharibi.

Usasa tunazungumzia mabadiliko ya dunia katika mfumo wa maisha ya mwanadamu na Umagharibi umesimama katika kupoteza asili ya Waafrika kama waanzilishi wa muziki huo.

Mambo hayo yanachangia katika mfumo wa mapambano ya maisha namna mwanadamu anavyopata maendeleo kadri siku zinavyosonga mbele na Umagharibi hutokana na kuelemewa na mfumo wa maisha ambao unapoteza asili na thamani ya utamaduni mwingine.

Hata wapenzi wanaoshangazwa na bifu kati ya wanamuziki wa hip hop au kwanini wanamuziki wa hip hop halisi (hardcore rap) wana misimamo inayoashiria mitafaruku hawajui kama hilo ni utamaduni wa hip hop.

Lakini kwa kutazama usasa siyo lazima kufuata utamaduni huu ikiwa rapa hana msimamo mkali juu ya hip hop.

Unaweza kupata tafsiri asilia kwamba hip hop ni imani, utamaduni, falsafa au itikadi juu ya ukombozi dhidi ya ukandamizaji wa aina mbalimbali katika jamii.

Hivyo hip hop siyo biashara kiasilia. Kama ndivyo basi tunaona wazi kuwa siyo kwamba wana hip hop wote wanafuata maadili asili ya muziki wenyewe kwani tayari tunaona Madee kaelemewa na usasa, ambayo inapigania kuficha asili ya muziki huo.

Muziki huu ulitumika ili kujinasua toka katika makucha ya ukandamizaji dhidi ya watu duni, hususani weusi. Sasa hip hop ilianzia wapi? kwanini hip hop iwe ni imani ya ukombozi na siyo biashara? ilikuwaje ikageuka na kuwa biashara?

Ni masuala ambayo yakipata majibu sahihi, baada ya kuifahamu kwa kina historia ya muziki wenyewe na asili yake ndefu, hapatakuwa tena na mjadala wa `Hip Hop Haiuzi`.


 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki  Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved.Design by Infocomtechnologies Limited.