Chakachaka kutua bongo Machi 29
Mwanamuziki mkongwe na mahiri wa Afrika Kusini Yvonne Chakachaka anatarajiwa kupamba ndani ya uzinduzi wa albamu ya kwanza ya kundi la kwaya la New Kitimutimu ya Dodoma, utakaofanyika Machi 30, mwaka huu, kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini.
New Kitimutimu ni kundi linaloundwa na waimbaji waliojitenga na mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili, Rose Mhando.
Mwenyekiti wa kundi hilo George Mgonhwa alisema kwamba Chakachaka atakanyaga ardhi ya bongo Machi 29, na siku hiyo hiyo atalonga na waandishi wa habari kabla ya kushiriki katika uzinduzi huo.
Mgonhwa alisema kuwa mipango yote ya Chakachaka kusindikiza uzinduzi huo imeshakamilika.
Kabla ya hapa Chakachaka alikuwa akiimba kanisani na siku za hivi karibuni amebadili mwelekeo na kuimba nyimbo za Injili, na amekwisharekodi albamu ya nyimbo za Injili.
Chakachaka amekuwa akishiriki katika matamasha mbalimbali ya nyimbo za Injili nchini Afrika Kusini, sambamba na kuwapokea waimbaji mbali mbali wa nyimbo hizo kutoka nje wanaokwenda kuimba nchini humo.
Mgonhwa alisema kuwa albamu watakayoizindua ina nyimbo nane na itabeba jina la ‘Vita hivi vyatoka wapi?’.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala