Sikurupuki tu, nafahamu nifanyacho!
Mwanamuziki mahiri wa injili Tanzania, Rose Muhando ameibuka na wimbo mpya unaokwenda kwa jina la ‘Jipange Sawa Sawa’, ikiwa ni maandalizi ya albamu mpya huku akitesa na kundi lake la Kitimtim.
Wimbo huo ni wa pili baada ya ‘Nibebe’, hivyo kufanya kuwa katika mstari ulionyooka na kuweza kuandaa albamu hiyo baadaye mwaka huu.
Msanii huyo aliweza tambulisha nyimbo hizo mbili kwenye tamasha la Pasaka, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee na kuweza kukonga nyoyo za mashabiki wake.
Mhando alisema kundi lake la Kitimtim liliweza kutia fora katika tamasha hilo, kwani amepania kufanya maajabu mwaka huu.
Alisema albamu yake hiyo mpya pamoja na kundi lake la Kitimtim itatia fora mwaka huu, kwani kuna wasanii wengi wa muziki huu na wanafanya kazi nzuri lakini mwaka huu amepania si kufanya kazi nzuri tu bali kazi bora.
Alisema kundi lake la Kitimtim aliloliunda miaka mitatu iliyopita, litazidi kufanya vema ndani ya Tanzania na hata nje ya mipaka kwani habahatishi bali analenga pale pale.
Alimalizia kwa kusema kwamba yeye hakurupuki kufanya kazi kwa kulipua, kwani anaandaa kile kilicho bora kwa jamii ili kuziteka nyoyo za wapenzi wa miondoko ya kumtukuza na kumsifu Mungu.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala