Leah Moudy atinga Idols!
Washiriki wawili wa shindano la Bongo Star Search (BSS) wa mwaka jana na mwaka huu...wamechaguliwa kuiwakilisha Bongo katika shindano la muziki la IDOLS kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini...shindalo lililodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Celtel.
Washiriki hao zao la BSS ni Leah Moudy...na Godfrey Gregory, mbali ya hao waliovuta hisia za wengi, wengine wawili watakaoiwakilisha nchi ni Linda Mwakalyelye na Doreen Aurelian ambao wote ni washindi wa Afrika Mashariki - East African Pop Idols.
Washiriki hao wanaungana na wengine kutoka nchi 22 na kufikisha idadi ya washiriki 100 ambao watakwenda Kenya katika mchujo mwingine unaotarajia kuanza Mei. Katika mchujuo huo watabakia washiriki 10 ambao wataingia fainali na mshindi atapatikana kwa kupigiwa kura na watazamaji.
Akizungumza wakati wa kutangaza washindi,Mkurugenzi wa Huduma ya Wateja ya Celtel, Lucille Aveva alisema kuwa kampuni yake inagharamia mafunzo ya washindi hao na kuwa tayari wameshaanza kunolewa kwenye kituo cha THT. “Kama mlivyoona washiriki wetu wanatakiwa kujirekebisha katika makosa kadhaa ambayo wametakiwa kuyafanya na muda ni mfupi, hivyo tumewapeleka THT ili wakapate mafunzo ya sauti na mambo mengine.
Pia kuna walimu kutoka Chuo Kikuu cha Dsm ambao nao wanawapa mafunzo washiriki hao. “Lakini kazi kubwa itakuwa ni katika kupiga kura za kutaka wawakilishi wetu waweze kufanya vizuri katika shindano hilo,” alisema. Awali Kampuni ya Celtel iliweka bayana kuwa imetenga Sh milioni 10 zitakazotumika kugharamia mafunzo ya wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Idols ili waweze kwenda kufanya vizuri.
Mshindi wa shindano hilo linaloandaliwa na M-net atapewa zawadi ya kuingia mkataba wa kurekodi na kampuni ya SONY BMG na zawadi ya dola za Marekani 80, 000 (zaidi ya Sh milioni 80). Nchi zinazoshiriki kwenye kinyang'anyiro hicho mbali na Tanzania ni Botswana, Burundi, Comoro, Djibouti, Ethiopia, Eritrea, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Reunion, Rwanda, Shelisheli, Somalia, Uswisi, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala