Udhalilishaji kijinsia umekuwa buguza kwa kukuza vipaji vya sanaa.
Kumekuwa na idadi ndogo ya wasanii wa kike katika medani ya muziki ukilinganisha na Wanaume na hilo halipingiki.
Wanawake ambao wamo katika aina mbalimbali za muziki wanaonekana kuwa na mchecheto mdogo ukilinganisha na wasanii wa kiume.
Sio kweli kwamba hawana uwezo wa kufanya sanaa zao kama ilivyo kwa Wanaume, kwani zipo sababu nyingi kwa baadhi ya wasanii hasa wale chipukizi waliyozipachika katika fani ya muziki.
Kimsingi muziki kama wa dansi huusisha idadi kubwa ya wanamuziki katika kundi moja, kwani unakuta waimbaji wa kike ni wachache na huku wengi wao kuonekana kushiriki katika unenguaji zaidi ya wengine.
Pia kuna sababu za kihistoria zinazowanyima wanawake nafasi ya kushiriki muziki ukiwemo mfumo dume, ambao umewanyima wengi wao haki ya kushiriki sanaa ya muziki kutokana na familia zao au hata waume zao kudhani kwamba kufanya muziki ni uhuni.
Vile vile zipo sababu zinazojificha ambazo siku hadi siku huwakatisha tamaa wanawake wengi kushiriki muziki, ambazo kimsingi huchangiwa na maumbile yao kama wanawake.
Mpaka msanii kuandika wimbo hadi kufanikiwa kusikika redioni zipo hatua nyingi ambazo hupitiwa na ambazo kimsingi huambatana na mitihani mikubwa yenye mtazamo wa udhalilishaji.
Hatua hizo huwafanya wanawake wengi hukosa ujasiriamali wa kukabiliana nazo na kujikuta wakijiingiza katika matendo yasiyofaa bila ridhaa yoyota ile, na wengine kuamua kukacha sanaa ili kufanya shughuli nyingine kwa kukwepa kudhalilika/kudhalilishwa.
Kama ilivyo makazini lakini katika sanaa inaweza kuwa zaidi kwa sababu huusicha wasichana wenye vipaji tu, ambao wengi wao hawana elimu ya kutosha ya kuwapa ujasiri wa kusimamia utu wao na wanachokifanya ni kuachana na fani husika au kukubali kuuza utu wao.
Wakati mwingine katika usambazaji wa mauzo ya albamu za muziki kumekuwapo na uchafu wa aina hiyo. Na siyo kweli kwamba wasanii wa kike huonekana kuwa duni katika fani mbalimbali bali hukumbana na vikwazo vya kila aina.
Siyo tu katika fani ya muziki kwani hata katika sanaa ya uigizaji mambo huelezewa kuwa mabaya zaidi, kwani inasemekana kuwa wamiliki wa makundi mengi yanayoonekana luningani hudai sana rushwa ya ngono hasa hasa kwa akinadada wanaomba nafasi katika makundi yao kama kigezo cha kuwapatia nafasi ya kuonekana.
Kwani baadhi ya wasanii wa kike wameweza kukiri kukosa nafasi hizo za kufika mbali licha ya kuwa na vipaji vikubwa kutokana tu na kukataa kwao kwa kujirahisishia kupata nafasi katika makundi husika.
Sasa wakati umefika kwa jamii kupinga kwa nguvu zote udhalilishaji ambao wanawake wamekuwa wakifanyiwa hasa wale wanaojihusisha na sanaa.
Zile mamlaka husika za serikali zinatakiwa kuwa karibu na makundi ya sanaa, hasa wanawake kwa kuwapatia semina mbalimbali ili wapate ujasiri wa kusema hapana katika mambo ya msingi ya kulinda utu wao.
 |

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala