Mtu mzima kudeal na machinga!
Ama kweli kimya kina mshindo! Usemi huo unadhirika kwa mambo mbalimbali, kwani ili jambo liwe zuri na lenye manufaa, halina budi kufanywa ama kutayarishwa kwa muda mrefu.
Hilo limetokea kwa mmoja wa waasisi wa muziki wa hip hop hapa nchini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama ‘Sugu’ ambaye kwa sasa anataka atambuliwe kwa jina la utani kama ‘Mtumzima’. Awali alianza kwa jina la ‘2 Proud’, kabla ya kuanza kujiita ‘Mr. II’.
Sugu amebainisha kuwa ujio wake wa sasa ni wa kivingine, kwani amekuja kwa mtindo wa kubuni njia mpya ya kuuza kazi zake kwa kuwashirikisha wamachinga ili kupunguza wizi uliokithiri wa kazi za wasanii nchini.
Ujio huo ni moja kati ya mikakati ya kupambana na kilio cha wasanii wengi nchini ambao wamekuwa wakilalamika kwa kutofaidika na jasho lao kutokana na kuibiwa kazi zao.
Anasema kwa sasa atakuwa akiwatumia wamachinga moja kwa moja kwa kuwapatia kazi zake halisi wazisambaze. “Nimeamua kutumia njia hii ili nipunguze lawama kwa wasambazaji ambao wamekuwa wakilalamikiwa kuwalipa wasanii fedha kidogo huku wao wakiingiza fedha nyingi…kujaribu si kushindwa na hapo ndipo nitakapojua ukweli, ” anasema.
Albamu hiyo ambayo ni ya kumi kwa msanii huyo tangu ajikite katika muziki inajulikana kama ‘VETO’, ambayo aliizindua Desemba 24 mwaka 2009 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee,jijini Dar es Salaam.
“Albamu yangu nitaisambaza kwa usimamizi wa hali ya juu kwa kufanya kazi bega kwa bega na wasambazaji wadogo wadogo ‘wamachinga’…hakuna kumwanini mtu kwa sasa… nitahakikisha inawafikia wote watakaoihitaji, iwe mjini ama vijijini”, anaongeza.
Akizungumzia kwa undani zaidi hatua hiyo mpaka kufikia maamuzi hayo, Sugu anasema kwamba awali alikuwa hafahamu wapi anapokwenda lakini kujituma kwake katika fani pamoja na kujaribu kila kitu ndiko kumemfikisha hapo alipo.
“Tulivyoanza tulikuwa hatujui tunakwenda wapi, lakini kuthubutu na kujiamini ndiyo kumetufikisha hapa tulipo sasa,” anasema.
Akizungumzia kuhusu mwelekeo wa muziki huo kwa sasa, anasema wasanii wengi wanafanya muziki kwa kuiga, jambo ambalo si zuri na halileti maendeleo katika medani hiyo.
“Napenda kuwaasa wasanii wanaochipukia wasifanye usanii kwa kumuiga fulani anafanya nini au anaimba vipi, ndiyo utoke, fanya kitu unachokipenda na unachomudu ili usije kuishiwa ubunifu,” anaongeza.
“Kila msanii ajiulize kwa wakati wake ametoa kazi gani ikamletea zogo mtaani, kuwa chachu ama kumletea misukosuko,” anasema.
Anaendelea kusema kuwa misukosuko ya hapa na pale ni jambo la kawaida, pia ni sehemu ya chachu kwenye gemu, kwani bila hiyo hakuna maendeleo, kama msanii hujawahi kukumbwa na misukosuko, basi uamini kuwa bado hujapata changamoto.
“Hivi wewe kupitia kazi yako hujawahi kupatwa na misukosuko ya kazi? na msanii yeyote anatakiwa afahamu kwamba asingeweza kufahamika bila ya kuwa msanii hivyo hatakiwi kukubali kuvunjika moyo,” anasema.
Kama hiyo haitoshi, mtu mzima Sugu amewaasa wasanii chipukizi kutunga mashairi yenye ukweli ili yawe funzo kwa jamii na kutoumiza vichwa vyao kwa kutafuta mashairi bomba wakati kuna mambo mengi yanayotokea katika jamii yanayopaswa kutungiwa mashairi na kutoa funzo kwa jamii.
Anaendelea kwa kusema: “Msanii anatakiwa atupe ‘experience’ ya ukweli, wasiumize vichwa katika kufikiria sana wakati umefika kila mtu apiganie haki kisanii kwa kutoa mashairi yatakayobaki mioyoni mwa watu na si mradi kuimba tu,” anasema.
Aidha, amesema kwamba anasikitika kuona kwamba hivi sasa wasanii hawana umoja, hivyo inakuwa vigumu kuweza kusaidiana.
“Hivi sasa wasanii hawana mshikamano, hivyo kuna umuhimu kwa kila kampuni kutoa udhamini kwa mtu yeyote atakayejitolea katika kuandaa kongamano la kuwakutanisha wasanii hasa wa muziki wa Bongo Flava, ambao ulishika chati zaidi katika miaka ya mwanzoni mwa 1990 hadi sasa.
Akijibu swali langu lililotaka kujua...mashabiki kutohudhuria kwa wingi kwenye onyesho lake la uzinduzi lililofanyia December, anasema kwamba ana imani kuwa halikutangazwa ipasavyo, kwani alisikitishwa na idadi ya mashabiki wachache waliojitokeza siku ile.
“Mimi siwezi kufanya shoo ikose mashabiki kama vile, kule ni kunidhalilisha, kwa sababu watu walikuwa hawana taarifa zozote za uzinduzi wangu, nilitarajia uzinduzi ule ungefunika shoo zangu zote nilizowahi kuzifanya huko nyuma kutokana na kimya kingi”, anaongeza.
“Simaanishi kama nimeshuka au wamefanikiwa kunishusha, nasisitiza mtu mzima dawa, ila ninacholalamika ni kwamba kwa nini jamii na wadau wangu hawakupewa taarifa ipasavyo?” anahoji.
Anasema kwamba kitendo hicho kina lengo la kuuporomosha muziki wa kizazi kipya, kwani vijana wengi wanachipuka hivi sasa na wala si kumshusha.
Sugu kama mmoja ya waasisi wa muziki nwa kizazi kipya, albamu yake ya kwanza aliitoa mwaka 1995, ikijulikana kama ‘Ni Mimi’, nyingine na miaka yakwe kwenye mabano ni ‘Ndani ya Bongo’ (1996), ‘Niite Mr. II’ (1998), ‘Nje ya Bongo’ (1999), ‘Millennium’ (2000), ‘Itikadi’ (2002), ‘Sugu’ (2004), ‘Coming of Age’au ‘Ujio wa Umri’(2006) na VETO (2009).

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala