Wakati homa ya uchaguzi mdogo wa Arumeru ikianza kupanda, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi, Uchumi na Fedha, Mwiguru Nchemba, amewaomba wanachama wa chama hicho wilayani Arumeru kumuepusha na kazi ngumu aliyoipata katika kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga, akisema kuwa licha ya ushindi, alipungua zaidi ya kilo saba kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa vyama vya upinzani.
Akiongea akiwa Arumeru, Nchemba aliyekuwa meneja wa kampeni katika uchaguzi wa Igunga, alisema wakati akikabidhiwa kazi hiyo alikuwa na zaidi ya kilo 97 lakini hadi uchaguzi unakamilika alibakiwa na kilo 90 pekee.
“Wana Arumeru nataka niwahakikishie jambo moja kuwa uchaguzi mdogo si lelemama, kuna kazi kubwa na inabidi kujiandaa kikamilifu kukabiliana na wenzetu ambao tayari wametamba kunyakua jimbo hili kutoka mikononi mwetu,” alisema Nchemba
Ikumbukwe kuwa mpinzani mkuu kwenye uchaguzi wa Igunga, kilikuwa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA).