Share |

Hatutaki kumuona Lema Meru - Wazee

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amemshauri Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuwaomba radhi wazee wa kimila wa kabila la Wameru ‘Washiri’ vinginevyo hali ni mbaya kwake na kundi lake.

Akiongea hayo jana wakati akizungumzia mambo ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Alisema maneno aliyoyaongea Lema siku ya maziko ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari, kiliwakera Washiri na kumtaka asikanyage jimbo hilo wakati wa kampeni.

Alisema yeye alikwenda katika jimbo hilo kuonanana wakuu wa Serikali na taasisi zake kupanga mkakati wa uchaguzi, lakini ghafla alikutana na wazee hao waliosema mbele yake, kuwa Mbunge huyo wa Arusha Mjini, hawataki kumwona katika kampeni, vingivevyo damu inaweza kumwagika juu yake.

"Washiri wamesema hawataki kumwona Lema katika kipindi cha kampeni kwani alileta dharau kubwa na utovu wa nidhamu siku ya maziko ya Sumari, hatua ambayo iliwakera wazee hao … ni busara tu, Lema kwenda kuwaomba radhi wazee hao kama anataka kufanya kampeni ya mgombea wa chama chake- Chadema,” alisema Tendwa.

Msajili alivitaka vyama vya siasa kuheshimu mila na desturi za makabila, ili kuepuka umwagaji damu na kushauri kuwa ni vema vyama vya siasa katika kampeni kuzingatia hilo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Meru, siku ya maziko ya aliyekuwa Mbunge wa Meru Jeremiah Sumari, Mh. Godbless Lema alisikika akisema kutokana na kifo Sumari jimbo hilo lazima lirudi CHADEMA, maneno ambayo yaliwakera wazee wa Kimeru.