Wakati mzimu wa kulipana posho ukiendelea kulitafuna Taifa, mapya yameibuka jana baada ya kubainika kuwa wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Mafuta Nchini (TPDC), wanatumia Sh. milioni 900 kwa mwaka kwa ajili ya kulipana posho za safari.
Hilo limeibuliwa kusikotegemewa baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), chini ya mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, kukutana na uongozi wa TPDC kwa ajili ya kuangalia mahesabu ya fedha wanazozipata kwa mwaka.
Zitto akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuahirisha kikao hicho kilichowaweka kiti moto TPDC, alisema kiasi hicho cha fedha wanachotumia kulipana posho za safari ni nusu ya mapato yote wanayolipwa na makampuni mbalimbali ya mafuta yaliyopo hapa nchini.
"Kamati yetu imeshtuka kusikia fedha nyingi kiasi hiki zinatumika kwa ajili ya kulipana posho za safari na mahojiano na hawa jamaa (TPDC) yalikuwa marefu na hatukuyamaliza hivyo tumeahirika na tumewaagiza watufuate Dodoma wiki ijayo," alisema
Alisema kwa mwaka wanapata mapato yanayofikia Sh. bilioni 1.8 na kwamba nusu ya fedha hizo zinapelekwa Wizara ya Nishati na Madini na zinazobaki wanazitumia kwa ajili kujineemesha kupitia posho za safari.
Zitto alisema kutokana na hatua hiyo na mambo mengine kamati yake iliamua kuahirisha kikao hicho na kuitaka TPDC, wiki ijayo iwafuate mjini Dodoma wakaendeleze kiti moto.