Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, iliwataka wabunge walitafakari suala hilo na ikiwezekana watumie busara kuachana nalo kwa sasa.
Nape aliwataka wabunge kufungua masikio na kusikiliza sauti za Watanzania ambao wamekuwa wakilalamikia nyongeza ya posho hizo ambazo katika siku za hivi karibuni zimezusha zogo kubwa.
“Wabunge wakiwa huko bungeni wana wawakilisha hawa Watanzania. Ni vizuri kusikiliza hiki kilio chao, si busara kupuuza kilio cha waliokupa dhamana ya kuwawakilisha. Tunawasihi waheshimiwa wabunge wetu nao walitafakari hili na kuona busara ya kuachana nalo kwa sasa,” alisema.
Mzozo wa posho mpya juzi uliingia katika hatua mpya baada ya Rais Kikwete kukana kubariki posho hizo, huku Spika akisisitiza kwamba Rais Kikwete ndiye alibariki posho hizo.
Kauli ya Makinda ilishabihiana na ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyewaeleza wahariri wiki iliyopita kwamba Rais Kikwete amelirejesha faili la suala hilo mezani kwake kwa ajili ya uamuzi; na baadaye alinukuliwa akisema lugha ile ile ya Makinda.