'Hayo ni madogo mno tuachane nayo'
Uamuzi wa Rais JK kuongea na wahariri wa vyombo vya habari hivi karibuni umeibua longolongo wa baadhi ya vile alivyoongelea.
Kwanza ni uamuzi wa kutupilia mbali tuhuma dhidi ya Rais Mstaafu Benny Mkapa zilizotoka katika gazeti la THISDAY kwamba alikuwa mjasiriamali wakati akiwa Ikulu.
JK alisema hivyo ni vitu vidogo vyenye nia ya kuchochea chuki na akatoa msimamo wake kuwa hatafuatilia tuhuma hizo.
JK alisema serikali yake haiko tayari kuanza kuwachunguza viongozi wastaafu kwa tuhuma za kusikia tu bila kuwa na uthibitisho wenye uhakika.
"Hivi kweli tuanze kumchunguza Mkapa eti kwa sababu alikopa benki na kulipa deni kabla ya muda aliopewa? Naomba tusifike huko kwani tutaanza kujenga utamaduni ambao si mzuri," aliongeza
Kingine Rais JK alichowataka Watanzania kufanya ni kujitokeza na kwenda kupima afya zao ili kujua hali zao na kujua namna ya kuishi kwa matumaini au kujilinda na maambukizi ya ukimwi. Na tuliunga mkono sana.
Ila tayari wapinzani wameshaanza kuwasha moto wakidai huo si uadilifu kwa Rais JK kufumbia macho vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya uongozi na huenda anafanya hivyo ili kujilinda na chochote kitakachoibuka akiwa madarakani.
Pia wapinzani walilotoka na kumtaka JK kuwaongoza Wabongo kwenda kupima ngoma na kutangaza majibu yake.
Lakini tunadhani wapinzani kama viongozi vilevile wangeweza nao kumwuunga mkono Rais kupima hali zao na kusaidia kupambana vilivyo kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.
Kwa hiyo si vibaya Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema na wenzake kujitokeza kupima ili kutoa mfano kwa wengine.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala