Wabunge nao kulamba mshiko zaidi
Maombi ya Wabunge kuongezewa posho mara tu walipotinga madarakani hatimaye yamesikilizwa na yapo katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2007/2008 katika baadhi ya vionjo vilivyomo.
Jumla ya sh. bilioni 42.5/- zimetengwa ili kuwawezesha Wabunge wetu kukizururisha kila kona ya majimbo yao wakisaidia vilivyo kutatua matatizo ya wananchi ndani ya mashangingi yao makubwa. Mshiko huo umeongezeka kutoka sh. bilioni 34.5/- walizotengewa mwaka jana.
Posho walizoongezewa ni mafuta ya kuvurumishia michuma yao kutoka lita 500 walizokuwa wanalipwa awali hadi kufikia lita 1,000 kwa mwezi.
Mafuta hayo ni pamoja na mafedha mengine waliyokuwa wanalipwa awali ya sh. milioni 1.2/- kama mshahara, nyingine sh. milioni 1.2/- ili ziwawezesha Waheshimiwa hao kuhudumia majimbo yao kikamilifu. Kumbuka mishiko hiyo unatoka kila mwisho wa mwezi.
Mshiko mwingine wanaokomba Wabunge ni wa vikao vya bunge ambapo hulipwa sh. 140,000/- kila siku wanayotinga Bungeni.
Hata hivyo bajeti hiyo imewakumbuka vilevile Wafanyakazi kwa kutenga sh bilioni 91.5 kama nyongeza za mishahara na bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu kupigiwa pande la sh. bilioni 54/- zaidi kukabiliana na mahitaji makubwa ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Mwaka jana bodi hiyo ilikuwa imetengewa sh. milioni 63.5/- na baadaye kupata nyongeza ya sh. bilioni 47/- baada ya fedha za awali kuwa kiduchu sana.
Sekta ingine iliyopata nyongeza ya mshiko katika bajeti ya mwaka huu ni JWTZ walioongezewa sh. bilioni 7/- kama posho ya mmango kwa kwa askari na kuongeza bajeti yao hadi kufikia sh. bilioni 199.8/-.
Bajeti hii kutoka kwa Waziri Wizara ya Fedha Zakia Meghji ilisomwa kwa Kamati ya Fedha na Uchumi na inatarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala