Unoko wa viza kwa wabongo waondolewa.
Ubalozi wa Marekani nchini umeamua kuondoa unoko wa viza kwa wabongo, kwa kurahisha utaratibu wake wa kutoa kwenda Marekani.
Uamuzi huo umetolewa katika ofisi za Ubalozi wa Marekani, na ofisa anayeshughulikia masuala ya viza, Robert Hannan,alisema kuwa kwa mwaka huu wanatarajia kutoa viza zaidi ya 5,000.
Hannan alizitaja juhudi muhimu zinazofanywa hivi sasa na ubalozi huo ili kurahisisha upatikanaji wa viza kwa watu wanaomba kuwa ni pamoja na kupunguza muda wa kusubiri mahojiano, ambako alisema kuwa kwa miezi 18 iliyopita waombaji walikuwa wanapewa ahadi ya kukutana na kufanyiwa mahojiano ndani ya siku mbili.
Hata hivyo, alisema kuwa hivi sasa hawajali sana maelezo
yanayotolewa na muombaji kwenye nyaraka, ila wanachoangalia sana ni uwezo wa kujieleza wa muombaji.
Alisema kuwa hivi sasa asilimia 75 ya watu wanaoomba viza hapa nchini kwenda nchini Marekani hawabaniwi.
Hata hivyo, aliwataka waombaji kuomba viza mapema miezi miwili,au minne kabla pamoja na kuwa na sababu muhimu ya kumfanya aombe.
“Kama kuna mtu anajua kuwa atakwenda kutembea Marekani, lazima aanze kufanya utaratibu hivi sasa, asisubiri barua ya mwaliko kutoka kwa ndugu yake au mawasiliano ya kibiashara, maombi yanapatikana kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu tanzania.usembassy.gov,” alisema.
Hannan alisema kuwa watu wengi huomba viza ya utalii na viza ya wanafunzi wanaokwenda kusoma nje lakini imekuwa ni usanii badala yake hujiingiza katika vitendo viovu kama vya kigaidi.
Tangazo la kulegeza taratibu za upatikanaji wa viza za Marekani linakuja siku chache tu tangu Rais wa nchi hiyo, George W. Bush alipofanya ziara ya siku nne nchini.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala