Vingunge dawa za kulevya waonja joto.
Rais JK, ameamua kutoendelea kula bati kwa kuwashughulikia
vingunge, wanaotuhumiwa kuhusika katika biashara haramu ya
uingizaji na uuzaji wa dawa za kulevya.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete, inatekelezwa kupitia mamlaka
zinazohusika na udhibiti wa dawa hizo, kutokana na majina ya wafanyabiashara hao yaliyowasilishwa kwake.
Maofisa wa kitengo cha polisi cha kudhibiti dawa hizo, na wale wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, walithibitisha kukamatwa kwa watu 100 wanaotuhumiwa kuhusika na biashara hiyo.
Walikuwa wanazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam , baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa kujenga uwezo wa kudhibiti biashara hiyo, uliofadhiliwa na Ubalozi wa Uingereza hapa nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya katika jeshi la polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Godfrey Nzowa, alisema miongoni mwa watuhumiwa hao, walifunguliwa mashtaka na wengine kuwa chini ya ungalizi wa mahakama.
Alisema dawa iliyobainika kutumiwa na wafanyabiashara hao, ni heroine, inayopatikana kwa urahisi katika nchi za Pakistan na Iran, kuliko Mandrax na Cocaine inayolimwa Brazil.
Naibu Balozi wa Uingereza hapa nchini, Bw. Tony Brennam, alisema mafunzo hayo yaliyowashirikisha maofisa kutoka taasisi kama polisi,Mamlaka ya Mapato (TRA) na uhamiaji, yana lengo la kuwajengea uwezo katika mbinu za kudhibiti biashara hiyo.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala