Tafuta DHWTangazaTuandikie
   
Wauaji watokomea na kichwa.

Ajuza mmoja mkazi wa Kijiji cha Madaho, Kata ya
Lunguya wilayani Kahama, alizikwa kiwiliwili tu
baada ya kuuawa kinyama kwa mapanga na kisha
wauaji hao kumkata kichwa na kutokomea nacho.

Mauaji hayo ya kinyama yanayoaminika kuwa
yalitokana na imani za kishirikina, yamezusha
gumzo kubwa kijijini hapo baada ya watu
wasiojulikana kumuua Bibi Kabula Ncheye (80),
kumkata kichwa na kuondoka nacho.

Habari kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho,
zilizothibitishwa na Diwani wa Kata hiyo,
Benedick Manwari, zilisema ajuza huyo aliuawa
Machi 8 majira ya saa mbili usiku, nyumbani
kwake wakati wakijianda kula chakula cha jioni.

Akisimulia mkasa huo, Manwari alisema kuwa
ajuza huyo akiwa nyumbani na wajukuu zake
wakiwa nje wanaota moto, walifika wanaume
wawili ambao waliomba maji ya kunywa. Mtu wa
kwanza baada ya kupokea maji hayo, aliyanusa na
kisha kuyamwaga chini na wa pili naye alifanya
hivyo hivyo.

Diwani huyo alisema walipomaliza kufanya hivyo
wauaji hao walianza kuwauliza familia ya bibi
huyo iwapo wanapika na kuuza pombe, baada ya
kujibiwa na wajukuu wake kuwa hawafanyi
biashara hiyo, walianza kuwamulika machoni kwa
tochi.

Wakati wanawamulika kwa tochi, walitokea
wanaume wengine wawili, hali iliyowatisha
wajukuu wa bibi Ncheye ambao walianza kukimbia
ovyo.

Baada ya wajukuu kukimbia, watu hao
walimkatama bibi huyo na kumchinja na
kuondoka na kichwa chake.

Alisema jitihada za kukitafuta kichwa hicho tangu
siku hiyo ya tukio hazikuzaa matunda na hivyo
kusababisha ajuza huyo kuzikwa kiwiliwili tu.



 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki |   Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved. Design by Infocomtechnologies Limited.