Maisha bora na ugumu wa maisha.
Pamoja na mwelekeo mzuri wa hali ya uchumi wa nchi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa taarifa inayowataka Wabongo kujiandaa kutokana na uwezekano mkubwa uliopo wa kupanda kwa gharama za maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya BoT inayohusu hali ya sera ya fedha kwa miezi sita iliyopita iliyotolewa mwishoni mwa Februari mwaka huu, uchumi wa Tanzania unakabiliwa na shinikizo kubwa litakalosababisha ongezeko la mfumuko wa bei na gharama za maisha.
"Katika miezi michache ijayo, shinikizo kwenye uchumi
litakalosababisha mfumuko wa bei litatokana na ongezeko la hivi karibuni la bei ya umeme, ongezeko la viwango vya mishahara na posho na kuendelea kwa ongezeko la bei ya petroli katika soko la kimataifa," ilieleza taarifa hiyo iliyopelekwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Mustafa Mkulo.
Hata hivyo, BoT imeainisha baadhi ya hatua ambazo zitachukuliwa ili kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha, ingawa baadhi ya hatua hizo zitazidisha makali ya maisha.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ili kukabiliana na tishio la mfumuko wa bei, Serikali itachukua hatua kali za kubana mzunguko wa fedha ili uendane na uzalishaji wa huduma na bidhaa.
Taarifa hiyo ilifafanua, kwamba hatua hiyo isipochukuliwa, mzunguko mkubwa wa fedha sokoni usioendana na kiwango cha uzalishaji, utageuka na kuvutia ongezeko zaidi la bei za bidhaa na huduma za ndani ya nchi.
Kuhusu hatua zitakazochukuliwa kupambana na baa la njaa, Serikali imeondoa ushuru wa kuagiza chakula na nafaka kutoka nje ya nchi ili kuvutia waagizaji kutoka sekta binafsi, wasaidie kupunguza uhaba wa chakula katika masoko mengine nchini.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala