TICTS kupelekwa Bungeni .
Suala la Kitengo cha Kupakua Makontena katika Bandari ya Dar (TICTS) kuongezewa muda wa mkataba wa pili kabla ya mkataba wa awali haujamalizika, sasa linatarajiwa kupelekwa katika kikao kijacho cha Bunge, wabunge wakitaka mkataba huo wa pili uvunjwe.
Sambamba na hilo, wabunge wanataka iundwe tume kuchunguza
mchakato mzima wa kuwaongezea muda kampuni hiyo wanayodai
haina ufanisi na waliohusika waanikwe hadharani.
TICTS iliyokodishwa kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2000,
iliongezewa muda wa mkataba mwaka 2005 ambako sasa
utamalizikia mwaka 2025.
“Kamati ya Miundombinu katika taarifa yake ya mwaka 2007
itakayoiwasilisha katika Bunge la mwezi ujao, inataka kufahamu sababu za mkataba huo kuongezewa muda kabla ya wa kwanza haujamalizika wakati ni kinyume cha taratibu na kutaka usitishwe katika muda uliobaki,” kilisema chanzo cha habari.
Katika maelezo yao, wabunge hao wanadai utendaji wa TICTS ni mbovu na hakuna sababu za kuendeleza mkataba, hivyo wameshauri kazi hiyo ipewe kampuni nyingine yenye uwezo.
Wanataka pia kipengele kinachowapa mamlaka TICTS ya
kuendesha kazi hiyo peke yao bila kuwapo ushindani kutoka kampuni nyingine kiondolewe, kwa imani ndicho kinachochangia kuzorotesha shughuli za kitengo hicho.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala