Tafuta DHWTangazaTuandikie
   
Trafiki wala rushwa kupigwa picha.

Sakata la madai ya askari wa usalama barabarani mkoani
Kilimanjaro kukithiri kwa vitendo vya kudai na kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa mabasi, limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Kikosi hicho nchini, James Kombe,kukunjua makucha.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki Kamanda Kombe aliomba msaada kwa wanahabari hao kwa kuwapiga trafiki watakaokuwa wakipokea rushwa kutoka kwa madereva wa mabasi ya abiria.

“Naombeni sana mlisaidie Jeshi la Polisi kupambana na tatizo hili, naombeni mahala popote mtakapowaona trafiki wanapokea rushwa, pigeni picha na mzitume kwangu moja kwa moja,” alisema Kamanda Kombe.

Mbali na hilo, alitoa ruhusa kwa abiria wanaotembea na simu zenye kamera kuwapiga picha askari hao pindi watakapowaona wakipokea rushwa kutoka kwa makondakta na madereva wa mabasi hayo ya abiria.

Pia amewaagiza na kuwaomba madereva wote wa mabasi ya abiria na wale wanaoendesha magari makubwa na madogo, kukataa kutoa hongo kwa askari hao na wakiombwa kwa nguvu, wawasiliane na makamanda wa polisi wa mikoa husika.

Hatua hiyo ya Kamanda Kombe inakuja siku chache baada ya
wasafirishaji katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kumuomba akutane nao ili wamweleze ufisadi uliokithiri unaofanywa na askari wa Kikosi cha Usalama barabarani katika mikoa hiyo.



 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki |   Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved. Design by Infocomtechnologies Limited.