bomoabomoa yazua maandamano hadi ikulu.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimedhamiria
kuandamana, ili kuelezea uvunjifu wa haki za binaadamu waliofanyiwa wakazi wa Tabata Dampo, Dar es Salaam.
Lengo la maandamano hayo ni kuishinikiza Serikali kutoa tamko kuhusu hatima ya wakazi hao ambao kwa karibu mwezi mmoja sasa hawana makazi.
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na chama hicho kwenda kwa
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred
Tibaigana na kusainiwa na David Kafulila, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa chama hicho, ilieleza maandamano hayo yataanzia Tabata kuelekea Ikulu.
Ilieleza maandamano hayo yatafanyika kesho kuanzia saa saba mchana yakiwa na lengo la kuuelezea umma uvunjifu wa haki za binadamu uliofanywa na Manispaa ya Ilala kwa wakazi hao.
“Tunatanguliza shukrani tukiamini utatoa ulinzi wa kutosha katika maandamano hayo ya amani hasa kwa kuzingatia kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya ujenzi wa demokrasia, utawala bora na uwajibikaji nchini,” ilieleza sehemu ya barua hiyo yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/KUH/18.
Katika bomoabomoa hiyo nyumba 96 zilivunjwa na askari wa
Manispaa ya Ilala na kuwaacha wakazi zaidi ya 500 wa eneo hilo bila makazi, hali inayowafanya waishi kwenye mazingira magumu.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, John Lubuva, amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tume huru iliyoteuliwa na Waziri Mkuu.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala