Mafua ya ndege kutinga Bongo?
Serikali imewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa wa mafua makali ya ndege nchini, kwa sababu ugonjwa huo kwa sasa umeshaingia Juba, kusini mwa Sudan, ambayo inapakana na Uganda na Kenya.
PM Mizengo Pinda, alibainisha hayo wakati akizindua Mpango wa Tahadhari na Udhibiti wa Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege, PM uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
“Tishio la kuingia na kuenea kwa ugonjwa huu nchini mwetu ni kubwa kuliko tulivyodhani siku za nyuma na hii inatokana na kama nilivyosema na ukweli ni kwamba ugonjwa umeingia kusini mwa Sudan.
“Hali hii inaashiria kuwa ugonjwa huu unaenea kwa kasi kubwa. Kutokana na ukweli huu, sasa hofu imezikumba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa huenda ukafika katika nchi hizi wakati wowote,” alisema Pinda.
Kwa mujibu wa waziri mkuu, kutokana na sababu hizo, kuna haja ya kuchukua tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuzuia kuingia na kusambaa.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Wanyama Ulimwenguni (OIE), ugonjwa huo ulianzia Hong Kong mwaka 1997 na kusambaa katika nchi 61, zikiwemo 11 za Bara la Afrika, ambazo ni Benin, Burkina Faso, Cameroon, Cote d’voire, Djibouti, Ghana, Niger, Nigeria, Misri Sudan
na Togo.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli, alisema kwa sasa bado ugonjwa huo haujafika Tanzania.
Aliongeza kuwa ili kuudhibiti, serikali imepiga marufuku uingizwaji wa nyama na ndege wanaosafirishwa kutoka nje.
Pamoja na mambo mengine, alisema kwa sasa serikali imeanzisha maabara ya kisasa yenye uwezo wa kuchunguza kuhusu kuwapo kwa ugonjwa huo.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala