Tafuta DHWTangazaTuandikie
   
MP,s wapinga michuma ya kifahari.

Baadhi ya wabunge wameitaka Wizara ya Fedha na Uchumi
kuachana na ununuzi wa michuma kifahari pamoja na misamaha ya kodi, wakisema kuwa maeneo hayo kwa kiasi kikubwa yanaipotezea serikali mapato.

Katika hoja zao, wabunge hao wanadai kuwa Wizara zinapopeleka bungeni kuomba kuidhinishiwa mapato na matumizi yao, huwa zinaweka ununuzi wa magari, lakini hazifafanui ni aina gani ya magari yanayonunuliwa.

“Hili eneo lina utata, kila wizara na idara inaamua kununua magari inayotaka, mengine yanaunuliwa hata hayaisaidii wizara husika bali kuingiza gharama zaidi,” alisema Mbunge wa Igalula, Tatu Ntimizi
(CCM), akizungumza katika mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG).

Walikuwa wanachangia katika hoja aliyoitoa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ambaye pamoja na mambo mengine,
aliwaeleza mipango ya serikali katika kupanua wigo wa kodi kwenye bajeti ijayo.

Ntimizi alitoa mfano kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iliwahi kununua magari ya kifahari aina ya Lexus, lakini muda mfupi baada ya magari hayo kufika, iligundulika hayafai kwa ajili ya ofisi hiyo hivyo yakakaa hapo bila kazi.

Alisema eneo hilo la ununuzi limekuwa kama mradi wa baadhi ya watu kula fedha za serikali kwa kununua magari ambayo wakati mwingine gharama zake ni zaidi ya matumizi ya wizara husika.

Katika ripoti yake ya hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, alisema kuwa ununuzi wa magari, samani na matengenezo ya magari ni maeneo makuu yanayoipoteza serikali mapato makubwa.

Mbunge wa Pangani, Mohamed Risherd (CCM), alihoji kuwa kuna baadhi ya idara za serikali ambazo huwa zinabakiza fedha, lakini wakati wa bajeti mpya huwa hazionyeshi fedha hizo zinapelekwa wapi.

“Katika vitabu ambavyo tunaletewa hizi fedha huwa hazionekani, huwa zinapelekwa wapi? Alihoji. Baadhi ya wabunge pia wametaka Ofisi ya CAG iondolewe Wizara ya Fedha na Uchumi, badala yake msimamizi wake liwe Bunge ili iweze kutekeleza majukumu yake vizuri.



 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki |   Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved. Design by Infocomtechnologies Limited.