Mwenye vilonga kupeta.
Kilio cha wananchi juu ya gharama za juu mno za kupiga simu kitapungua mara baada ya serikali kukamilisha mpango wake wa kujenga mkonga maalum badala ya kutumia mawasiliano ya satelaiti yanayokuza gharama na kuwakamua watumiaji.
Rais Jakaya Kikwete, kwa mara ya kwanza, aliweka wazi mpango huo wa serikali wa kujenga mkonga maalum kwa lengo la kujaribu kuwapunguzia makali wananchi wanaotumia huduma ya simu.
Kwa mujibu wa Rais, matumizi ya satelaiti katika mawasiliano ya simu, ndiyo chanzo cha kuwapo kwa gharama kubwa za upigaji simu tofauti na nchi nyingine zikiwamo nchi za Ulaya.
Ingawa hakutaja ni lini mpango huo utakuwa tayari na wala hatua iliyokwishafikiwa hadi sasa katika utengenezaji wa mkonga huo, lakini aliwaambia wananchi wa Iramba Mashariki katika mkutano wa hadhara jana mchana kuwa mradi huo utakapokamilika, gharama za simu za Tanzania zitakuwa sawa na gharama ya huduma hiyo katika nchi nyingine duniani, likiwamo bara la Ulaya.
Alilazimika kutoa maelezo hayo wakati akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mawasiliano ya simu nchini tangu aingie madarakani takribani miaka miwili na nusu iliyopita.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala