Haya ni majigambo ama!
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, amesema serikali ya Bongo imechukua hatua kadhaa ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa nchiikiwa ni pamoja na kuliondoa taifa katika kundi la nchi tatu maskini zaidi duniani.
Miongoni mwa hatua hizo zilizochukuliwa, ni pamoja na kuanzisha hatua za kudhibiti utoroshaji wa fedha nje ya nchi unaofanywa na watu wasio waaminifu, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwahimiza wananchi wanaoishi mamtoni kuwekeza fedha zao katika benki za hapa nchini.
Pamoja na hatua hizo, serikali imefanikiwa kuongeza pato la taifa kwa kiasi cha shilingi trilioni saba kutoka sh trilioni 18 za mwaka 2006 hadi kufikia sh trilioni 25 mwaka huu.
Hatua hiyo ambayo inahusisha kuimarika kwa huduma za kijamii na kiuchumi, itaiwezesha Tanzania kuondoka katika nafasi ya tatu kwa umasikini duniani hadi kufikia nafasi ya 14 katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, alisema hatua hizo pia zitawezesha kuongezeka kwa pato la Mtanzania kutoka wastani wa dola 480,000 mwaka 2006 hadi kufikia dola 631,000.
Alisema pato la taifa limekuwa likiongezeka zaidi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2006 hadi sasa na mwaka jana lilifikia sh trilioni 21 sambamba na pato la Mtanzania lililofikia sh 545,455 kwa mwaka.
Mkulo alisema, kabla ya kuongezeka kwa pato hilo, mwaka 1992 pato la taifa lilikuwa sh trilioni 7.6 na pato la Mtanzania lilikuwa halizidi sh 350,000 kwa mwaka.
Alisema kukua kwa uchumi kunatokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi pamoja na kuboreka kwa huduma mbalimbali za jamii kiasi cha kuwafanya watu watumie muda mwingi kufanya shughuli za kuwaingiza kipato, hivyo kujiongezea kipato na pato la taifa kwa ujumla.
“Nchi yetu ni ya tatu kwa umasikini duniani, lakini kutokana na kuongezeka kwa pato letu, nina hakika tutapanda hadi kufikia nafasi ya 14 katika miaka miwili ijayo na kadri tutakavyozidi kufanya vizuri ndivyo tutakavyoondoka katika lindi hilo,” alisema Mkulo.
Alisema kukua huko kwa pato la taifa hakuwezi kuonekana moja kwa moja kwa wananchi, bali ni kuimarika kwa miundombinu ya barabara, maji, hospitali na huduma nyinginezo ambazo zitasaidia shughuli za uchumi kufanyika kwa urahisi zaidi.
“Najua watu watakuwa wakiuliza kama pato la taifa linakua, iweje maisha ya wananchi yaendelee kuwa chini, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa, fedha hizo zinaonekana zaidi katika uboreshaji wa miundombinu, jambo litakalosaidia nchi kuondoka katika nafasi za chini kwa nchi zilizo kwenye mstari wa umasikini,” alisema Waziri Mkulo.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala