Zombe apagawa
Mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, jana alionekana kuchanganyikiwa baada ya kufikishwa katika msitu wa Pande, uliopo Mbezi, nje kidogo ya Jiji la Dar
es Salaam ambako kunadaiwa kufanyika mauaji ya watu hao.
Muda wote wa kusikilizwa kwa kesi hiyo jana katika eneo hilo, Zombe alionekana mtu mwenye jazba huku akiuliza maswali mwenyewe bila kupitia kwa mawakili wake.
Mara zote aliporuhusiwa na Jaji Kiongozi, Salum Masati kuuliza maswali, baada ya shahidi wa 30, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora (RPC), Edson Mmari, kutoa ushahidi wake, Zombe alikana kuhusika na kutolijua eneo hilo.
Maswali mengi aliyokuwa akiuliza Zombe, yalikataliwa na Jaji Masati na kumweleza kwamba yanapaswa kuulizwa wakati shahidi huyo atakapomaliza kuhojiwa na Wakili wa Serikali, Alexander Mzikila.
“Walah mimi sikuwa eneo la tukio na huku sikujui kabisa, shahidi naomba uniambie katika sisi watuhumiwa 13 ni nani uliyeambiwa alikuwa eneo la tukio wakati mauaji hayo yanafanyika?” alihoji Zombe.
Mahakama ilihamia kwa muda katika eneo hilo, kutokana na maelezo ya mshitakiwa wa 11, Rashidi Lema, anayodaiwa kutoa Mmari, kwamba mauaji hayo yalikuwa ni ya kupangwa na waliouawa hawakuwa majambazi.
Wakati Zombe akiuliza maswali mengi ya kujitetea, mshitakiwa mwenzake huyo (Lema) alisikika akimtaka Zombe aeleze baada ya kukamilika kwa mauaji hayo alikunywa bia ngapi.
“Elezea yote kama hujawahi kufika katika eneo hili na baada ya tukio hilo ulijipongeza kwa kunywa bia ngapi?” alisikika Lema akisema kwa sauti ya chini.
Lema, alisikika akitoa maneno hayo kwa sauti ya chini na baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa karibu naye, wakati Mmari alipokuwa akionyesha eneo ambalo marehemu hao walikuwa wamelazwa na kufyatuliwa risasi hadi mauti yalipowafika.
Katika msitu wa Pande, shahidi huyo alidai hapo ndipo walipochukua sampuli ya udongo uliokuwa umeganda na damu na kuupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kujua kama damu iliyokuwa hapo ilikuwa ya mnyama au binadamu. Mkemia Mkuu katika ushahidi wake,
alieleza kuwa damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu.
Msafara huo ulipokuwa ukielekea eneo la msitu wa Pande, wananchi waliojipanga barabarani walisikika wakisema: “Na wao lazima wauawe huko huko, wasirudi wazima hao, kwa kuwa wamewaua wenzao, Ni lazima wakauawe jamani, hakuna kuwaachia na wasirudi na wao wakauonje umauti huko,” walisikika wakisema wananchi hao.
Baadhi ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali, Mzikila na shahidi Mmari eneo la msitu wa Pande, yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Hebu shahidi ielezee mahakama ni nini hasa lengo la Rashid (mshitakiwa wa 11) kukuleta huku wakati mnafanya upelelezi wenu?
Shahidi: Lengo la Rashid lilikuwa ni kuona eneo la tukio ambalo wafanyabiashara hao wanaodaiwa kuwa majambazi waliletwa na kuuawa
mmoja badala mwingine, kwa kulazwa chini na kufyatuliwa risasi.
Wakili: Mlipofika eneo hili mliona nini na kukichukua kama kielelezo katika kesi hii?
Shahidi: Tuliona damu ikiwa imeganda chini ya ardhi na maganda mawili ya risasi ambavyo vyote vilichukuliwa kama vielelezo katika kesi hii.
Alidai Lema alimweleza kuwa baada ya kufikishwa eneo hilo akiwa na dereva Koplo Rajab, walishuhudia Saad Alawi (mshitakiwa ambaye
hajapatikana) akiwaua wafanyabiashara hao kwa kuwafyatulia risasi.
Shahidi Mmari akimnukuu mshitakiwa Lema alidai Alawi ndiye aliyehusika na mauaji hayo na si yeye.
Awali, mahakama hiyo ilikwenda nyumbani kwa shahidi wa pili, Bernadeta Ngonyani eneo la Sinza C, sehemu ambako kunadaiwa marehemu
hao walikamatwa na polisi kabla ya kupelekwa sehemu isiyojulikana hadi walipokuwa maiti.
Katika eneo hilo, shahidi Mmari, alieleza mshitakiwa Lema alimueleza jinsi wafanyabiashara hao walivyokamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na
kupakizwa katika gari la Polisi la Kituo cha Chuo Kikuu, Dar es Salaam.
Baada ya kuondoka eneo la Sinza C, mahakama ilikwenda eneo la ukuta wa posta, eneo ambalo lilidaiwa na watuhumiwa hao kuwa
mashambulizi kati yao na waliodaiwa kuwa ni majambazi yalifanyika hapo, hadi kujeruhiwa kwa majambazi hao na kufia njiani wakati
wakipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Katika ukuta wa posta, shahidi Mmari aliieleza mahakama kuwa alichoona wakati wa kufanya uchunguzi huo ilikuwa ni matundu manne ya risasi
lakini kwa sasa ameona tofauti kwa kuwa matundu yanayoonekana ni zaidi ya 10 na kwamba kwa upande wa pili wa ukuta huo pia kuna
matundu mengine.
Mahakama ikiwa eneo hilo, Zombe alionekana kuwa mkali huku mara kadhaa akivua miwani na kuivaa na kumuomba Jaji Masati kutoa ruhusa
kwa askari yeyote ambaye si mshitakiwa akabidhiwe silaha na kufyatua risasi, ili matundu yaliyopo ukutani hapo yaonyeshwe iwapo yatakuwa
na tofauti na yaliyopo hapo.
“Mheshimiwa Jaji, kama haya matundu si ya risasi basi aje askari yeyote ambaye si mtuhumiwa afyatue risasi hapa halafu tufananishe kama
haya si ya risasi,” alieleza Zombe huku jaji akikataa ushauri huo na kusema endapo watafanya hivyo watawashtua raia waliokuwa jirani na eneo
hilo.
Baada ya kutoka eneo hilo, majira ya saa 5:11 asubuhi, mahakama ilikwenda eneo la Konoike ya zamani, Barabara ya Sam Nujoma, sehemu
ambayo watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi, ambao kwa sasa ni marehemu ndiko wanakodaiwa walifanya uporaji katika gari la Kampuni ya
Bidco Oil.
Katika eneo hilo, Wakili wa utetezi, Majura Magafu, alimuuliza shahidi ni kitu gani kilichomfanya kukumbuka eneo hilo wakati kuna mabadiliko
makubwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara unaoendelea.
Akijibu swali hilo, shahidi Mmari, alieleza anakumbukumbu na eneo hilo kwa kuwa kulikuwa na ofisi ya ujenzi wa barabara ya Konoike, hivyo
hata wangekarabati kwa kiasi gani asingeweza kulisahau.
Wakati wa msafara huo wa magari zaidi 20 uliokuwa na ulinzi mkali huku ukiongozwa na ving’ora, wananchi wengi walionekana kuwapo
pembezoni mwa barabara na kutoa kauli mbalimbali ambazo zilionyesha kuchukizwa na kitendo cha mauji ya watu hao.
Majira ya saa 8:20, mahakama ilihamia tena katika eneo la Bunju eneo ambalo mtuhumiwa 11 alidai akiwa pamoja na Saad Alawi, walikwenda
kupiga risasi hewani kwa ajili ya kupata maganda matupu ya risasi zilizotumika ili kuweza kuweka rekodi katika daftari la kusajili risasi hizo
ambazo Janurai 14 zilirudishwa zikiwa hazijatumika hata moja.
Wakili wa Serikali Mizikila alimuuliza shahidi huyo kama kuna ushahidi wowote waliokuwa wameupata eneo la tukio wakati wanafanya upelelezi
huo.
Mmari alijibu hakuna ushahidi walioupata hapo ila Lema aliwaambia kuwa maganda yaliyokuwa yametumika katika eneo hilo alimkabidhi Koplo
Rajabu ambaye pia ni mtuhumiwa.
Mara baada ya shahidi kumaliza kutoa ushahidi wake akiwa katika eneo la Bunju, Jaji Salum Masati, aliahirisha kesi hiyo ambayo itaendelea
leo kwa ajili ya kufungwa kwa ushahidi wa Mmari, ikiwa mawakili wa upande wa utetezi watamuuliza maswali.
Mahakama hiyo ilimalizia msafara wake kwa kwenda eneo la Bunju ambako kunadaiwa mshitakiwa Lema na Alawi walitumwa na mshitakiwa
wa pili, Christopher Bageni kufyatua risasi hewani, ili kupata ushahidi wa maganda ya risasi.
Shahidi huyo, alidai kuwa alielezwa na Lema kwamba alifyatua risasi tatu na Alawi risasi sita na kisha wakapeleka Kituo cha Polisi Oysterbay
kwa ajili ya kufuta kumbukumbu za awali (Januari 14, 2006) ambayo ilionyesha risasi walizochukua zilikuwa hazijatumika.
Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Christopher Bageni, Noel Leonard, Jane Andrew, Moris Nyangelela,
Emmanuel Mabula, Felix Cedrix, Koplo Michael Abeneth, Koplo Rajabu, PC Rashid Lema na Festus Bwabisabi.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka juzi, ambapo waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini na dereva
teksi.
Marehemu hao ni Ephraim Chigumbi, Mathius Lunkombe, na dereva teksi Juma Ndugu.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo, ambako shahidi huyo anatarajiwa kuhojiwa na mawakili wa upande wa utetezi.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala