Tafuta DHWTangazaTuandikie
   
Wafanyakazi waichimba serikali mkwara

Jinamizi la migomo ambalo lilipozwa kwa muda na hotuba aliyoitoa bungeni Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni na ahadi nyingine za serikali, linaonekana kuanza kurejea kwa kasi, baada ya wafanyakazi katika maeneo muhimu kijamii na kiuchumi kutangaza azima yao ya kugoma katika kipindi cha siku chache zijazo.

Wafanyakazi waliotangaza kugoma jana ni madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambao wameshtushwa baada ya kubaini kutokuwapo kwa nyongeza zozote katika mishahara yao ya Agosti mwaka huu, waliyopokea hivi karibuni.

Hatua kama hiyo ya wafanyakazi wa Muhimbili ilitangazwa jana pia na wenzao wa Shirika la Reli nchini (TRAWU) ambao walitoa siku 11 kwa menejimenti yao wakilalamikia kutotekelezwa kwa ahadi ya kuanza kuwalipa viwango vipya vya mishahara kuanzia Agosti mwaka huu.

Kwa upande wao wale wa Muhimbili, wao walitoa siku moja hadi kesho Ijumaa, wakiitaka serikali iwe imewalipa nyongeza za mishahara mipya kama ilivyoahidi.

Katika Hospitali ya Muhimbili, huduma nyingi zilisimama kwa muda jana baada ya baadhi ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine hospitalini hapo, kukusanyika mbele ya sehemu ya mapokezi ya zamani kwa saa kadhaa, wakijadiliana hatima ya mishahara yao.

Baadhi ya wafanyakazi hao, walisikika wakisema katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, walikuwa na wakati mgumu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, lakini walikuwa na matarajiao makubwa ya kupata mishahara mipya baada ya serikali kuahidi kufanya hivyo.

Akizungumza mbele wafanyakazi hao, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Serikali Kuu na Afya (TUGHE) tawi la Muhimbili, Nusura Barakabitse, alisema uvumilivu wao umefikia kikomo na kusisitiza kuwa hakuna mfanyakazi atakayeingia kazini kuanzia siku hiyo.



 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki |   Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved. Design by Infocomtechnologies Limited.