maisha ya wabongo msoto-JK.
Pamoja na kupokea pongezi za China kuhusu kukua vizuri na haraka kwa uchumi wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete amesema Tanzania ni nchi masikini na maisha ya wananchi bado ni magumu.
Amesema kuwa kupanda mno kwa bei za mafuta katika miaka ya karibuni, pia kumechangia kuzidisha ugumu wa maisha kwa wananchi.
“Ni kweli Tanzania ni nchi ya amani na isiyoyumba. Uchumi wetu umekuwa unakua kwa wastani wa asilimia saba kwa miaka kadhaa sasa.
Lakini bado maisha ya wananchi wetu ni magumu. Bado yetu ni nchi masikini,” Rais Kikwete aliuambia ujumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China jana.
“Pato la wastani ya wananchi wetu ni dola za Marekani 500 tu, na ongezeko la bei la mafuta katika miaka ya karibuni limeyafanya maisha ya wananchi wetu kuwa magumu zaidi,” alisema. Rais Kikwete alikuwa anazungumza na ujumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China wakati alipokutana nao kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Rais Kikwete alikuwa njiani kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara ya Mkoa wa Manyara. Ujumbe huo uliokuwa katika ziara ya siku tatu nchini kwa mwaliko wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliondoka baada ya mazungumzo hayo kwenda Uganda kuendelea na ziara yake katika Afrika. Uliwasili nchini kutokea Afrika Kusini Jumanne, na baada ya Uganda unakwenda Gabon na Nigeria.
Rais Kikwete alitoa ufafanuzi huo kuhusu tafsiri ya uchumi wa Tanzania baada ya kiongozi wa ujumbe huo, He Yong, ambaye ni Katibu wa Sekretariati ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti kuimwagia sifa nyingi Tanzania, uchumi wake na uongozi wa Rais Kikwete. He Yong alisema: “Yenu ni jamii iliyotulia, isiyoyumba.
Tanzania ni moja ya nchi zenye uchumi zinazokua haraka kwenye bara hili. Yote hayo yametokana na uongozi wako imara ambao umeongeza
uwezo wa utawala bora wa nchi yenu.” “Ni jambo la kutia moyo na kufurahisha kwamba kwa miaka 10 sasa, uchumi wenu umekuwa unakua
haraka na kwenda mbele. Tunapenda kuelezea husuda yetu kwa uongozi wako ambao umepelekea mafanikio haya yote,” alisema Katibu huyo.
Rais Kikwete pia alitumia nafasi ya mazungumzo hayo kumweleza kwa undani hali ya kiuchumi nchini, na hasa hatua zipi Tanzania inastahili
kuzichukua kuongeza kasi ya kukua kwa sekta ya kilimo, ambayo alisema ndiyo itakuwa mkombozi wa kweli kweli wa Mtanzania. Rais pia
alimwelezea He Yong kuhusu hali ya Tazara, akisema reli hiyo imekuwa inakabiliwa na matatizo mengi kwa sababu ya menejimenti
isiyoridhisha.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala