Kweli huu ni mwaka wa shetani kwa Vyuo Vikuu
Jamani hii sasa kali kwa upande wa Vyuo vikuu vya hapa nchini, kweli ni mwaka wa shetani kwa Vyuo hivyo kukumbwa na sakata zima la mgomo.
Kwani wanafunzi wa mwaka wa kwanza 595 ndani ya Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara mkoani Kilimanjaro (MUCCoBS), kimechukua jukumu la kuwatimua wanafunzi hao kutokana na kuanzisha mgomo chuoni hapo.
Mbali na sakata la mgomo wanafunzi hao wametuhumiwa kwa kuhatarisha maisha ya baadhi ya wanafunzi wenzao wa mwaka wa pili, na wa tatu sambamba na wahadhiri chuoni hapo baada ya kuwamwagia mchanga na kuwarushia mawe wakiwa darasani.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Profesa Suleiman Chambo alisema kwamba kutokana na mgomo huo, menejimenti iliamua kuwasimamisha masomo wanafunzi hao kwa muda usiojulikana.
"Wanafunzi wa mwaka wa kwanza walipoona wenzao wa mwaka wa pili na tatu hawawaungi mkono, waliamua kuwafuata madarasani na kuwamwagia mchanga na kuwarushia mawe huku mhadhiri mmoja akiwa darasani, Profesa Temba, ambaye alinusurika kipigo na ilimbidi kuingia chini ya meza ili kujinusuru," alisema.
Wanafunzi hao hawana madai ya msingi na kwamba moja ya madai yao ni kuishinikiza Serikali kuwalipia mikopo kwa asilimia 100, huku madai mengine ni kuwaunga mkono wanafunzi wenzao katika vyuo vikuu vilivyofungwa.
Alisema wameamua kuwarudisha nyumbani kwa muda usiojulikana, na watakaporudi itawapasa waandike barua wathibitishe kulipa ada kwa asilimia 100.
Profesa huyo alisema wanafunzi hao wanatakiwa waombe ruhusa ya kurudi chuoni, na kufuata taratibu za chuo na walete vyeti vya kuonesha kwamba wana sifa za kurudia shahada wanayosomea.
Alidai kuwa wanafunzi hao pia walitishia maisha ya Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Zamu Mlimila ambaye alilazimika kuokolewa na polisi baada ya wanafunzi kumzonga kwa lengo la kumshinikiza atangaze mgomo chuoni hapo.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala