Tafuta DHWTangazaTuandikie
   
Utata watanda kifo cha mfanyabiashara Tunduma

Mwili wa mfanyabiashara,Frank Mwachembe anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari Polisi PC Justine umeendelea kusota chumba cha maiti Tunduma kusubiri uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo hicho.

Hatua hiyo imetokana na kuibuka utata kutoka kwa ndugu na kudai wana shaka kuhusu mazingira ya kifo cha ndugu yao kwani eneo la tukio, hakukuwa na damu na kwamba huenda aliuawa kwa kunyongwa kisha kuchomwa kitu ubavuni kuhalalisha kuwa aliuawa kwa risasi.

Akizungumza sababu za kuchelewa kwa mazishi, mdogo wa marehemu alisema wamehofu baada ya kuona mwili wa marehemu na jeraha lililodhaniwa kuwa limetokana na risasi .

Amesema wameuona mwili wa marehemu ukiwa na jeraha dogo lakini tundu la risasi halikuonekana lilipotokea upande wa pili na wao kama familia, wanatilia shaka kifo hicho.

Alisema wanapata shaka pia kwani baada ya ndugu yao kufa, polisi walizuia watu kuingia chumba cha maiti hadi wananchi walipovunja mlango na dirisha na kuuona mwili ndipo walipoanza maandamano kushinikiza Polisi aliyedaiwa kuua, auawe.

Ameeleza kuwa ili kujiridhisha kama familia wamemtafuta daktari wao ambapo upande wa Polisi umesema utatuma wataalamu kutoka Dar es Salaam kuchunguza mauaji hayo.

Mke wa marehemu, Lucia Anthony, alisema kwamba alisikia milio ya risasi na baadaye honi na mngurumo wa gari la mumewe hivyo aliposikia taarifa kuwa kuna mtu amepigwa risasi na kufa, alijiuliza huenda si mumewe bali ni mtu mwingine aliyekuwa akiendesha gari la mumewe.


"Tunataka haki itendeke na ukweli ujulikane na ielezwe bayana chanzo cha mauaji hayo kama kulikuwa na uadui kati ya huyo askari na mume wangu iwekwe wazi ," alisema.



 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki |   Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved. Design by Infocomtechnologies Limited.