Tafuta DHWTangazaTuandikie
Wakuvanga a.k.a Waziri Mkuu!!




Isaya Mwakilasa a.k.a Wakuvanga, ni miongoni mwa waigizaji maarufu, aliyejizolea sifa kemkem kutokana na umahiri wake wa kuigiza katika kipindi cha vichekesho cha The Comedy, kinachorushwa kila Alhamisi kupitia kituo cha East Africa Television (EATV) cha Dar es Salaam.


Wakuvanga anapouvaa uwaziri mkuu'Ulowasa'

Hii Title ya Uwaziri mkuu naamanisha Lowasa alipachikwa baada ya kumuigiza kuanzia sauti hadi umbile kwa kuweza kuvaa uhusuka ambapo alifanikiwa kuteka halaiki

Wakuvanga anasema kwamba, kipindi cha The Comedy kimemsaidia kumwepusha na kujiunga katika magenge ya kihuni na badala yake kuangalia zaidi maisha yake ya mbele.


Anasema anakishukuru kituo cha televisheni ya EATV kwa kuanzisha kipindi cha The Comedy, kwani kwa kushiriki kwake kwa muda mfupi, tayari anajiona kupata mafanikio ikiwamo kujizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki.


Wakuvanga, anasema safari yake ya kimaisha hadi alipofikia sasa, ilikumbwa na mateso na mahangaiko ya kila aina.

KUHUSU MAISHA YAKE


“Baada ya kutengana na mama, baba akaoa mke mwingine na kuzaa naye watoto saba,” anasema Wakuvanga.



Baba yake alikuwa ni mwajiriwa katika Jeshi la Polisi na alikuwa ni mtu anayejulikana na kuheshimika.


Anasema wakati yeye akinyanyasika, wenzake walikuwa wakipewa kila aina ya huduma waliyohitaji kutoka kwa baba yake.


“Vitendo hivi kwa kweli vilikuwa vikiniumiza roho sana na kujiuliza kwa nini baba alikuwa akifanya hivyo, nilijiuliza maswali mengi na kufikiria pia kuwa inawezekana yeye siye baba yangu mzazi.


“Unyama wake nafikiri ulimuhuzunisha hata mke wake (mama yake wa kambo), kwani kuna wakati alikuwa akinionea huruma na kudiriki kuninunulia nguo za shule kwa hela zake ndogo alizokuwa akizipata katika biashara yake ya kuuza ndizi mbivu nyumbani,” anasema.


Wakuvanga anasema mwaka 1993, akiwa darasa la nne katika Shule ya Msingi ya Mwenge ‘B’ huko Sumbawanga, baada ya kuchoshwa na manyanyaso ya baba yake, aliamua kutoroka nyumbani kwao na kwenda kuwafuata baba zake wakubwa waliokuwa wakiishi mkoani Mbeya.


Akielezea kuhusu safari yake hadi kufika mkoani Mbeya, anasema siku hiyo aliondoka nyumbani kwao saa 11 asubuhi kabla watu hawajaamka.


Hata hivyo, anasema kutokana na maeneo waliyokuwa wakiishi kuwa karibu na mpakani mwa Tanzania na Zambia, ilimchukua muda wa saa tisa hadi kuifikia barabara kuu ambako magari huwa yanapita.


Anasema kutokana na kutembea mwendo mrefu akiwa anaisaka barabara hiyo, alishindwa kuendelea na safari na kuweka kituo kijiji kilichoitwa Layela.


Alipofika kijijini hapo, alienda kwa mjumbe wa nyumba kumi ambaye anasema hamkumbuki jina lake.

KUMBE USANII ALIANZA LONGI

“Kutokana na usanii kuwa kwenye damu toka utotoni, ilibidi pale nifanye usanii. Nilimdanganya mjumbe kwamba nimetoka nyumbani na nimemuacha baba yu mgonjwa na hivyo natakiwa kwenda Mbeya kumchukua shangazi kwa ajili ya kuja kumuuguza.


“Maneno yangu haya yalimtoa machozi mjumbe kutokana na kunihurumia umri wangu, kwani nilikuwa bado mdogo ukilinganisha na majukumu niliyokuwa nayo,” anasema.


Hata hivyo anasema pamoja na kumuelezea mjumbe yote hayo, hakukumbuka kumuuliza kama ana nauli ya kumfikisha Mbeya jambo ambalo hata yeye hakutaka kuulizwa kwani kama ilivyo watu wa kijijini, wangeweza kupitisha michango nyumba hadi nyumba na kusababisha hata watu wa nyumbani kwao kujua kwamba ametoroka.


“Mimi nilichokuwa nahitaji hapa ni malazi tu na siku iliyofuata niliamshwa asubuhi na mapema, nikanywa chai na kusindikizwa hadi barabarani kwa ajili ya kupanda basi.


“Wakati tukiwa tumeanza kushika pori, kondakta alianza kupita kwa abiria kukusanya nauli… akili yangu hapa ikaanza kufanya kazi harakaharaka, aliponifikia, nikamdanganya kwamba baba yangu mdogo ambaye alikuwa trafiki mkoani Mbeya ndiye aliyenituma nipande halafu nikifika kituo cha mabasi atawapa hela yao.


“Nashukuru Mungu alikubali bila kusita… baba yangu huyo trafiki walikuwa wakimfahamu, lakini mimi mwenyewe hata nilikuwa simjui na nilipata ujasiri wa kusema hivyo kutokana na stori alizokuwa anatupa baba nyumbani kuwa tuna baba yetu mdogo ambaye ni trafiki mkoani Mbeya,” anasema.


Hata hivyo, anasema walipofika kituoni, alishuka kama abiria wengine na kondakta wala hakumuuliza chochote.


“Kutokana na mimi kutokuwa mwenyeji katika mkoa huu, ilibidi niende kituo cha polisi na nilipomuulizia baba yangu huyo nikaambiwa kwamba alishahamishiwa wilayani Chunya.


Baada ya kupewa majibu hayo, Wakuvanga anasema akakumbuka tena kuwa ana baba yake mkubwa ambaye ni Padri na ndipo akili ilipomtuma kwenda makanisani na kumuulizia na kutokana na ukoo wa Mwakilasa kujulikana sana mkoani Mbeya katika kuuliza aliweza kumpata na akamsimulia mambo yote aliyokuwa akifanyiwa na baba yake.


Anasema baba yake mkubwa naye akawa anasubiri labda ndugu yake angeweza kumpigia simu kumtaarifu juu ya kupotea kwake kutokana na kutomuona nyumbani, lakini haikuwa hivyo kwani ilipita siku, wiki hadi mwezi ndipo akaamua kumpigia simu mwenyewe na alipomuuliza kuwa wanaendeleaje huko nyumbani, alimjibu hawajambo pasipo hata kumwambia kupotea kwake, ndipo akajua kweli ndugu yake hampendi mwanae.


Kutokana na kulithibitisha hilo, baba mkubwa huyo aliamua kumpeleka shule na kuanza darasa la tano kwani katika mtihani wake wa darasa la nne alifanya vizuri.


Anasema wakati akiwa Mbeya, alikuwa bado na kiu ya kumuona mama yake, kitu ambacho baba yake mkubwa hakutaka kukisikia na kumtaka kama atataka kumuona mama yake amtaarifu kwanza baba yake au la amrudishe Sumbawanga.


Siku moja Wakuvanga anasema akiwa katika matembezi, alikutana na msichana ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani wakati mama yake akiwa hajaachika kwa baba yake.


Anasema yeye hakumkumbuka, lakini msichana yule alimkumbuka na kuanza kumsimulia jinsi mama yake anavyojitahidi kila awezalo ili aweze kuonana naye bila ya kufanikiwa.


“Bado nilivyoenda na msichana huyu kwa baba mkubwa ili aniombee ruhusa ya kwenda kumuona mama yangu ambaye wakati huo alikuwa akiishi Iringa, nilikataliwa… nikaamua kutoroka na yule dada.


“Tulipofika Iringa nyumbani kwa mama, aliponiona tu alilia kama mtu aliyepata taarifa ya msiba,” anasema.


Anasema kutokana na kumpata mama yake, hakuona tena haja ya kurudi kwa baba yake mkubwa, akamuomba mama yake amfanyie utaratibu wa kumuhamisha shule ili aweze kuishi naye.


“Kweli, mama alinikubalia, lakini alipoomba msaada kwa baba mkubwa kuhusu uhamisho wa shule, alimkatalia kutokana na kukasirishwa kwa kitendo changu cha kumtoroka, hivyo ilibidi mama ahangaike mwenyewe hadi alipofanikiwa, nikarudia darasa la tano katika Shule ya Msingi Mkunyugu iliyopo mkoani Iringa na mwaka 1996 niliweza kuhitimu elimu yangu ya msingi,” anasema.


Baada ya kumaliza darasa la saba, mama yake alimtaka aende akamsalimie baba yake na kusahau mambo yote mabaya ambayo alitendewa.


“Nilikubali aliyoniambia mama, nikaenda kwa baba, lakini cha kushangaza pamoja na kukaa kote kwa baba hadi matokeo yakatoka ambayo hayakuwa mazuri, baba hakuniuliza lolote juu ya kuendelea na elimu ya sekondari, hivyo nikaamua kurudi zangu kwa mama.


“Baada ya kurudi, mama aliniuliza ningependa kufanya nini kwa kipindi kile, nikamjibu kuwa nataka kufanya biashara.


“Naamini kweli uchungu wa mwana aujuae mama, kwani alinipa fedha taslimu sh 200,000. Lakini kutokana na akili ya kitoto niliyokuwa nayo kwa wakati huo, sikuweza kuzifanyia jambo lolote la maana fedha zile, nilizitumia na marafiki zangu katika starehe mbalimbali,”anasema.


Mwaka 1998 mama yake akampeleka katika Shule ya Seminari Migoli iliyopo Mtera mkoani Iringa, lakini alipofika kidato cha tatu mwaka 2000, alitoroka kutokana na kushindwa kuishi maisha ya kiseminari, kwani yeye alikuwa akipenda kuwa muigizaji na shule hii haikuwa na mambo hayo.


Anasema fedha yote ya matumizi ya shule ambayo alikuwa akitumiwa ndiyo aliyoitumia kama nauli ya kutorokea Dar es Salaam ambako alifikia kwa baba yake mkubwa mwingine aliyekuwa akifanya kazi Wizara ya Afya kama daktari, ambaye alikuwa Mlokole na hivyo kumfanya naye aanze kuishi maisha ya Kilokole.


Lakini huko sasa akaweza kushiriki katika kwaya mbalimbali, maigizo ya kanisani vitu ambavyo ndivyo alikuwa akiviwania siku zote.

Ze comedy !!

KUANZA USANII RASMI

Kutokana na kufahamiana na waimbaji wenzake katika kwaya, walikuwa wakisikia sehemu ambayo inataka muigizaji wanamwambia na mwaka 2002 akajiunga na kundi la sanaa la Victoria Arts Group ambalo lengo lake lilikuwa ni kurusha vipindi vyake katika kituo cha ITV, lakini hata hivyo hakikufanikiwa kufanya hivyo.


Mwaka 2003 ndipo alipohamia katika kikundi cha Kidedea na kuwa kama mwalimu wa waigizaji wa kundi hilo hadi mwaka 2006 alipoacha na kujiunga na kundi la Mizengwe, yote ikiwa ni katika kutafuta maslahi.


Anasema toka alipohamia Mizengwe alijiona kuwa tofauti kwani aliweza kujifunza mambo mengi ambayo alikuwa hayajui kutoka kwa wakongwe wa kuigiza aliokutana nao huko na kumfanya kuwa bora zaidi.


Anasema wakati akiwa Mizengwe pamoja na kina Zembwela, waliweza kuigiza katika kipindi cha The Comedy ambapo baadaye Zembwela na wenzake Mkwere, Bi Kiroboto, Masele walijitoa kutokana na kushindwana na uongozi wa EATV katika malipo.


Anasema baada ya kina Zembwela kuondoka, yeye na Masanja ndio wakawa vinara wa kundi hilo ambapo yeye ni Mweyekiti huku Masanja akiwa Katibu.


“Ninamuamini sana Masanja, kwani hata kama watu wengine hawatakuwepo sisi wenyewe tunaweza kuendesha kipindi na kikaweza kwenda hewani, huyu mtu mimi namwita ‘Spea Malaya’ kwani anaweza kuigiza nafasi yoyote ile atakayopangiwa,” anasema.


Kuhusu malengo, Wakuvanga anasema lengo la The Comedy ni kuwa kikundi bora cha usanii kama lilivyo kundi la Parapanda na pia kuifanya The Comedy kuwa kampuni inayojitegemea.


Pia hivi sasa amegundua kuwa shule ni muhimu katika maisha ya mtu wa kawaida na hasa msanii kwa kuwa bila shule hakuna jambo lolote la maana ambalo litawezekana.


Licha ya kupania kusoma masomo ya sekondari, pia ana mpango wa kusoma fani ya kompyuta ili aweze kwenda na wakati.

MALENGO
Anasema malengo mengine ya The Comedy, ni kutoa albamu ya rap katini itakayoitwa ‘Ugali’, ambayo itakuwa katika kaseti za kawaida na ‘CD’.


Anasema katika albamu hii, kila kitu watakifananisha na ugali kutokana na uzuri utakaopatikana na wameamua kutumia jina la ugali kwani ndicho chakula kikuu katika makabila yote ya Afrika Mashariki.


Mambo ambayo anasema hayapendi katika maisha yake ni kusimangwa, ndiyo maana aliamua kuondoka kwa baba yake kwa ajili ya masimango.


Huyo ndiye Mwaluvanga ambaye sasa hivi anaishi na mwanakwaya mwenzake kama mtu na kaka yake hiyo ni kutokabna na kumpa hifadhi tangu alipoibiwa samani za nyumbani kwake.

Endelea kuzuru ukurasa huu kucheki makala za crew nzima ya ZE COMEDY.




 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 Mtumie Rafiki |   Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved.Design by Infocomtechnologies Limited.