Bandari ya Dar wanacheza
Huduma za kuingia meli bandarini, kupakua kontena na hatimaye wenye mizigo yao kuondoka au kuisafirisha kumeelemewa kwa foleni ndefu ya muda sasa.
Tatizo la foleni bandarini limekuwa kubwa na hivi sasa meli zinazotinga bandarini zikiwa na kontena za kushusha katika bandari ya Dar, zinasubiri kwa siku 6 hadi 10 kupakia mzigo.
Hivi sasa Mamlaka ya Bandari Tanzania -TPA imepigwa mkwara wa kudaiwa Vessel Delay Surcharge -VDS ya dola za Marekani 10,000 hadi 15,000 kwa siku moja kutokana na ucheleweshaji wa meli hizo zaidi ya siku zilizotarajiwa kupakua mizigo.
Gharama hizo zitazidi kuongezeka endapo foleni hiyo itaendelea bandarini Dar na wenye meli kuhisi kuwa wanapata hasara kwa kuwa katika mlolongo huo mrefu usio na muda maalum.
Baadhi ya meli zilizotakiwa kupakua mizigo yake Dar hivi sasa zinaelekezwa Mombasa, Kenya kupakua mizigo yake na hivyo kuongeza gharama kwa wenye mizigo ya kuisafirisha tena kwa barabara au meli kwenda Dar.
Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kenya, -KPA, Twalib Khamis
amethibitisha kuongezeka kwa mizigo mingi lakini uwezo wao mkubwa umewezesha kukabiliana na hali hiyo kwani wana vifaa vya kisasa na eneo kubwa la kuhifadhi kontena zipatazo 13,000.
Wahusika Wakuu bandarini Dar, wanaishia kurushiana mpira kati ya TPA na Tanzania International Container Terminal Services -TICTS, ila tatizo linadaiwa kuwa ni upungufu wa vifaa vya kisasa vyenye kasi ya kuendana na wingi wa mizigo mingi na mikubwa.
Bandari ya Dar yenyewe ina uwezo wa kuhifadhi kontena 6000 tu na imekuwa inafanya kazi chini ya kiwango kutokana na ukosefu wa vitendea kazi ikilinganishwa na vile vilivyopo katika bandari ya Mombasa.
Karibuni Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Baharini -SUMATRA
ilipendekeza kutumika kwa eneo la Ubungo kuhifadhia kontena
nyingine zipatazo 4,000 lakini TICTS imekuwa inajivuta kufanya hivyo kutokana na kinachodaiwa kukwepa gharama za ziada kutoka bandarini (hadi Ubungo).
Mizigo yote; yaani ile inayoingia nchini na ile inayosafirishwa kwenda nje imekuwa inacheleweshwa kuanzia Novemba mwaka 2006 na hivyo kuathiri uchumi wa nchi vibaya huku wafanyabiashara wakilalamika bila kusikilizwa kama vile mbuzi anayepigiwa gitaa.
Baadhi ya kampuni za Clearing & Fowarding zimekuwa zikilalamikia mizigo yao iliyokwama bandarini tangu January 4 mwaka huu huku watendaji wakijivuta kana kwamba hawaathiriki na hali hiyo kabisa wakati ukweli ni kwamba uchumi wa nchi nzima unaathirika.
Jitihada za kumpata msemaji yeyote wa TICTS hazikufanikiwa kwani mwenye ruksa ya kutoa kauli, Meneja Mkuu David Cotty alikuwa nje ya ofisi.
Wadau kibao wa Mawakala wa Meli -TSAA, TPA, na Tanzania
Freight Forwarders Association TAFFA kwa sasa wanahangaika kwa nguvu kujaribu kurekebisha hali lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote yaliyoonekana.
Lakini katika hali ya kunawa mikono TPA imekuwa inarusha matangazo kibao kuashiria kuwa hali ni shwari kwa upande wao na kuliacha soo hilo kwa TICTS, kampuni iliyoshinda bingo ya kuendesha shughuli za mizigo bandarini.
Longolongo la pande hizi mbili limezidi kuongezeka na hadi sasa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge ameingilia kati na kuitaka TPA kuchangamka na kurekebisha hali hiyo mara moja.
Amewataka wahusika kumpatia sababu kamili zinazosababisha tatizo hili badala ya longolongo lisilo na maelezo rasmi kutoka kwa wahusika.
Hali hii inatokea wakati Dar ndio karibu na vibosile wote wa nchi walipo, na hali hii imekuwa inasuasua hivi tangu mwaka jana na hakuna lolote la maana linalofanyika zaidi ya longolongo la hapa na pale.
Kwani TICTS ni nani, watuwekee mtimanyongo kama huu katika
bandari yetu? Jamani ina maana tumefikia mahali hata kazi zetu za ndani zinatushinda kufanya, -kupakua, kupakia mizigo na kushughulikia uchukuaji wa mizigo?
Iweje wenzetu Mombasa watupige bao kiasi hicho? Au tusema
wanatumia mganga gani wa kienyeji?

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala