Tafuta DHWTangazaTuandikie
Kukubaliana kutokukubaliana

Ni miaka mingi imepita ila kwangu inaonekana ni kama siku chache tu. Kila siku nawaza na kuwazua nikifikiria mambo yaleyale tu.

Matukio na maisha ya uanafunzi hayakomi kuvuruga mfumo na mpango wangu wa kuwaza na kuamua.

Kila siku ninayokumbana na mitihani ya shule na ya maisha, sikosi kukumbuka maisha ya shule ya msingi.

Kipindi ambacho nilifundishwa mambo mengi sana ninayoyajua leo.

Kipindi ambacho niliadhibiwa na mtu ambaye hakuwa ndugu wala mzazi wangu. Kipindi ambacho nilifundishwa kuomba ruhusa kabla sijatenda au kusema jambo lolote darasani.

Kipindi ambacho nilifundishwa kwa mara ya kwanza kuwa binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. Kipindi ambacho nilifundishwa lugha ya wazungu.

Katika yote niliyojifunza shule ya msingi, ninalolikumbuka zaidi ni mbinu ya ufundishaji aliyoitumia mwalimu wa kiingereza. Ili kuhakisha kwamba kila mmoja wetu anaongea angalau neno moja la kiingereza, mwalimu wangu alianzisha mijadala mbalimbali darasani ambayo kila mmoja wetu alitakiwa kushiriki.

Mwalimu aliita hii mijadala � debates - na moja ya masharti na sheria za mijadala hii; ni ruhusa ya kila mmoja wetu kusema neno lolote la kiingereza ili kuchangia mjadala bila kujali makosa na mpangilio wa sentensi.

Mbinu hii ya mwalimu ilifanikiwa sana kwani baada ya muda mfupi kila mtu alikuwa anaweza kusema angalau maneno kumi ya kingereza.

Kwangu mimi na baadhi ya wanafunzi wenzangu; mwalimu wetu wa kiingereza alikuwa ametufumbua macho na kujenga picha kubwa kuhusu mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu; Tulijifunza kuwa binadamu aweza kufanya kitu chochote kama akipewa nafasi na akiruhusiwa kufanya makosa wakati wa majaribio.

Mwalimu alituruhusu kupendekeza mada za debates, kuchagua makundi mawili yatakayopingana kwa hoja, na kujiunga na kundi mojawapo kati ya hayo mawili. Jambo lingine kubwa tulilojifunza kutoka kwa mwalimu ni sheria namba mbili ya mjadala ambayo iliruhusu watu kubishana kwa utulivu na amani bila ugomvi.

Tulitakiwa wote kufuata sheria kuu inayoongoza debates zote duniani inayowataka na kuwaruhusu wana mijadala kukubaliana kutokubaliana (agree to disagree).

Ndio; kukubaliana kutokubaliana. Sheria ambayo wanasiasa wengi leo hii Afrika wameisahau. Leo hii Afrika mwanasiasa akitofautiana sera na mwenzake, anakimbilia msituni kuanzisha vita.

Wanajeshi wakipitana kimawazo na viongozi wanasiasa, kinachofuatia ni mapinduzi. Mbona Waafrika hatukubali kutofautiana kifikara? Utakuta kiongozi anatishia watu kuwa akishindwa uchaguzi basi nchi yote itatumbukia katika vita na matatizo kibao. Haya yote ni ya nini?

Kwanini leo hii tusikubaliane kuwa tutaendesha mijadala inayohusu nchi yetu bila hofu kuwa wanaopinga watajikuta matatani. Ninadhani kuwa; sasa hivi ni wakati mwafaka kwa watanzania na waafrika wote kuamua kukubaliana kutokubaliana (agree to disagree) kila mara inapobidi.

Sera ya kukubaliana kutokubaliana ndio njia pekee itakayowaruhusu wabunge wa CCM kuikosoa serikali bila hofu. Sera hii itafanya baadhi yetu wanachama wa CCM kukemea baadhi ya maovu yanayofanywa na serikali bila hofu ya kuitwa wasaliti na wapinzani.

Sera hii itafanya wanasiasa wa vyama vyote vya siasa nchini kuonekana kama watu safi na wazalendo wa kweli kila mara wanapoikosoa serikali.

Mbinu hii itawakumbusha watanzania na waafrika umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani hata kama hawakubaliani katika misimamo yao ya kidini.

Msomaji wangu wa makala hii, jiulize kuwa utafanya nini kuwashawishi wenzako wenye mipango ya kutumia nguvu (force) kueneza ajenda, sera, dini, na imani zao kwa wenzao wasiokubaliana nazo.

MUNGU ibariki Afrika, MUNGU ibariki Tanzania.

Magabe Kibiti



 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 

Mtumie Rafiki

 Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved.Design by Infocomtechnologies Limited.