PM awazindua Bandari Dar
Tusitumie msemo wa punda haendi ila kwa mjeledi kwani wengine wataanza kulalamika kwamba tunatumia lugha mbaya, si uungwana mengine mengi.
Lakini ndio kilichotokea kwani hata wiki haijaisha vizuri tayari agizo la Waziri Mkuu Edward Lowassa kwa bandari ya Dar kufanya kazi masaa 24 lishaanza kuzaa matunda.
Iweje hawakugundua hili, iweje wakalie makontena ya watu wanaohitaji mizigo yao chap chap kwa ajili ya biashara na foleni ndefu za malori yanayosubiri mizigo hilo hatujui.
Wingi wa makontena bandari ulikuwa mkubwa hadi baadhi ya
makontena kuanza kuhamishiwa katika yard nyingine zilizoko Ubungo ili zihifadhiwe.
Kwani tatizo lilikuwa nini? Hakuna cha maana ila kila mmoja atasingizia hili na lile ili mradi hakuna aliyekubali kuwa anahusika.
Kitengo cha Huduma ya Makontena TICTS kilikuwa kinadai kutokuwa na vifaa vya kutosha na vya kisasa kukabiliana na wingi wa makontena yanayoshuka bandarini kila siku.
TISCAN - Kitengo cha ukaguzi wa mizigo wao walikuwa na longolongo kuwa mashine yao kila baada ya muda, inafaa ipumzishwe, si unajua tena ili kupooza mashine na Dar ilivyo na joto kali.
Mamlaka ya Mapato Tanzania kwao halikosekani jambo manake
wakikushushia hesabu zao mwanangu lazima urudi kwenu mwenyewe ukatie akili.
Wenye meli walikuwa ni zogo kila mara na Mamlaka ya Bandari
kutokana na kutakiwa kukaa foleni ya muda mrefu na hivyo kuongeza gharama zaidi ikilinganishwa na bandari ya Mombasa Kenya.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya meli kupakulia mizigo yao Mombasa hivyo kuongeza gharama wateja waliotakiwa kusafirisha mizigo yao kwa barabara kutoka Mombasa kuja nchini.
Malalamiko ya wateja yalikuwa kibao kutokana na gharama za
kuhifadhi kontena kuwa juu kutokana na kukaa muda mrefu bandarini kwa ukiritimba usiyo na mpango.
Tatizo lingine walilolalamika wateja ni tabia ya wakaguzi hao kujifanya kuulizia bei za bidhaa zinazotinga bandarini kutoka nje ili kuhakikisha na zile zilizotajwa na wahusika.
Licha ya kudhihirisha kwamba hawana bei maalum ya ushuru wa
bidhaa, utaratibu huu huchukua muda mrefu na hivyo kuongeza foleni ya kontena na mizigo mingine mingi bandarini.
PM Lowassa ametinga Bandari ya Dar na kutoa agizo hali hiyo
ibadilike na wadau wote wafanye kazi saa 24 kuondoa kero hiyo.
Hivi sasa TRA, Mamlaka ya Bandari, TICTS na TISCAN wanapiga mzigo wa kufa mtu na huku matangazo yakisisitiza kuwa kazi ni masaa 24.
TRA imetoa tangazo jinsi inavyotekeleza agizo bila kulala katika vituo vya gate namba 5 na 8, na vituo vingine vyote vya ukaguzi bandarini.
Mabadiliko tayari yanaonekana kwani zile foleni ndefu za malori yanayosubiri mizigo hakuna tena, kwani yanapita tu sha sha bila ya kokoro za zamani.
Sasa yote haya yanadhihirisha kuwa watu wakiamulia jambo linawezekana, ila sasa kwa Vibosile wa bandari walitakiwa kujua hayo kabla ya PM Lowassa hajatumia bakora yake.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala