Wabunge wetu wametuangusha
Imani yetu katika maamuzi haya ni kwamba, Watanzania tumeibiwa mali na viongozi wetu walioamua kuitumia vibaya dhamana ya madaraka tuliyowapa.
Kikao cha Bunge la Bajeti kiko katika hatu za mwisho mwisho mjini Dodoma na dalili zinaendelea kuonyesha kuwa, wabunge wanakaribia kuondoka Dodoma wakiwa wamezungumza na kupitisha maamuzi mengi tu mazito.
Pamoja na kukiri kuwa Bunge limeendelea kuweka rekodi mpya kila wakati, bado tunaendelea kulalamika kuwa limemalizika likiwa limeacha pasipo kujadiliwa kwa baadhi ya masuala ya msingi kabisa.
Ingawa limepitisha makadirio na matumizi ya wizara takriban zote, Bunge hili limeshindwa kujadili na kufikia hitimisho katika masuala mengi ya msingi.
Kama lilivyoshindwa kufikia maamuzi mazito ya pamoja katika masuala ya mgogoro wa Reginald Mengi na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, sakasaka ya Richmond na baadaye Dowans, mikataba ya madini na mengine mengi, bado limeendelea kukwama kutumalizia suala la uuzwaji wa nyumba za serikali kwa baadhi ya watumishi wa umma.
Kimsingi Bunge hilo pia, limeshindwa kujadili au japo kudodosa kuhusu ulipofikia uamuzi wa serikali wa kuzirejesha baadhi ya nyumba hizo ambazo ziliuzwa kwa viongozi wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Hii hasa ndiyo hoja kuu ya maoni haya.
Kwetu sisi wa Tanzania Daima, kama tulivyopata kusema huko nyuma, ukimya huu wa wabunge wetu waliokuwa na fursa nyingi za kulivalia njuga suala hili, hata kama ikibidi kuandaa hoja binafsi, ni wa kukatisha tamaa.
Wabunge machachari wa aina ya kina Zitto Kabwe, Halima Mdee, Lucas Selelii Hamad Rashid Mohammed na wengine wengi, tumewasikia katika mambo mengine ya msingi na baadhi yao wakifikia hata hatua kuandaa hoja kwenye masuala mengine isipokuwa hili la nyumba zetu.
Tunasema ni wa kukatisha tamaa kwa sababu suala hili ni moja ya mambo ambayo kwa kiwango kikubwa yalipingwa na watu wengi wakati wa utekelezwaji wake, hata kufikia hatua ya malalamiko haya kumfikia Rais Kikwete.
Mbele ya waandishi wa habari, Kikwete alilitangazia taifa hili, mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana kuwa, tayari serikali ilikuwa imeshaanza kuchukua hatua ambazo zitawezesha kurejeshwa kwa baadhi ya nyumba hizo za serikali ambazo alisema ziliuzwa kwa makosa.
Ingawa tulikuwa miongoni mwa Watanzania walioipokea kauli hiyo ya Kikwete kwa mikono, miwili, msimamo wetu tangu wakati huo umekuwa wazi kabisa kwamba, msamiati wa ‘baadhi ya nyumba’ unapaswa kuondolewa na badala yake urejeshwaji unapaswa kuwa wa ‘nyumba zote’ zilizouzwa.
Tusema hivyo tukiamini kwa dhati kuwa, uamuzi mzima wa kuziuza nyumba hizo ulifanywa pasipo kuweka mbele masilahi ya taifa na hivyo unapaswa kufutwa ili kumaliza fedheha hiyo ya kihistoria ambayo tutaendelea kuilalamikia siku nenda siku rudi.
Tunaamini unyeti wa maeneo zilikojengwa nyumba hizo, umuhimu wa nyumba zenyewe na ukweli kwamba, uongozi ni dhana ya kupokezana vijiti kama alivyopata kusema Rais Kikwete, uamuzi wowote wa kuipokonya serikali rasilimali yake muhimu unapaswa kufutwa pasipo kuangalia matokeo ya kufanya hivyo. Tulitegemea wabunge wangeliona hili.
Tunahitimisha maoni yetu, tukiwashitaki wabunge wetu kwa wananchi, pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi kuwa, wote wamekuwa ama wakibebwa na hoja za kujiimarisha majimboni, au zile za msimu na kusahau kuwa bado kuna maamuzi mengine ya siku za nyuma kama hili la kuuziana nyumba, ambalo lingali likitutesa. Wabunge wametuangusha.
Tanzania Daima

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala