Tafuta DHWTangazaTuandikie
Ajali za barabarani zithibitiwe

Ajali mbaya zimelikumba taifa katika siku za hivi karibuni, huku ile iliyotokea maeneo ya Mbarali mkoani Mbeya ikihusisha basi la Sabco, ikiwa ndiyo inayoongoza kwa kuua watu wengi zaidi.

Taarifa za awali za kipolisi, zinaonyesha kuwa, dereva wa basi hilo la Sabco ndiye ambaye kwa kiwango kikubwa alikuwa chanzo cha ajali hiyo kutokana na kuendesha gari kwa mwendo wa hatari sambamba na kuchukua uamuzi mbaya.

Ajali hiyo inatokea wakati huu taifa linapojiandaa kuingia katika Wiki ya Nenda kwa Usalama, ambayo pamoja na mambo mengine imekuwa ikihimiza haja ya madereva kuendesha magari yao kwa uangalifu.

Aidha, ajali hiyo inatokea miezi si mingi tangu polisi wa baadhi ya mikoa nchini waanzishe utaratibu wa kuyasindikiza mabasi ya abiria wa masafa marefu hadi katika mipaka ya mikoa yao, ili kuwachunga madereva wasiozingatia sheria za barabarani.

Leo hii baada ya polisi mkoani Pwani kwa mfano kutangaza utaratibu huo miezi kadhaa iliyopita, zile taarifa za mara kwa mara za mabasi kupata ajali mbaya katika mkoa huo zimepungua kwa kiwango kikubwa kwa muda sasa.

Uamuzi huo wa polisi ambao sisi tulieleza mapema kabisa kuunga mkono, ulitangazwa na aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ephraim Mrema, miezi kadhaa baada ya Mkoa wa Iringa kuchukua hatua kama hizo.

Kila mmoja anajua kuwa, Kamanda Mrema alitangaza uamuzi huo wakati barabara kuu ipitayo katika mkoa huo inayoliunganisha Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, likiwa limeshachukua sifa ya kuwa eneo hatari kusafiri.

Watanzania wanaofuatilia mambo na watu wanaosafiri kwa njia ya barabara hiyo ni mashahidi kwamba, Pwani kama yalivyo maeneo kadhaa mengine hapa nchini, imekuwa ikichukuliwa na watu wengi kuwa ndicho kitovu cha ajali, hususan zile zinazohusisha magari ya abiria.

Hali hii ya masikitisho, kwa miaka mingi imelifanya eneo lote inakopita barabara kuu mkoani Pwani kuwa ni moja ya maeneo ya maafa ambayo ilisababisha hospitali ya mkoa huo kuwa maarufu kwa kutibu majeruhi na kupokea maiti wengi kila mara kutokana na wingi wa ajali hizo.

Kukithiri kwa ajali katika eneo hilo ndiko ambako wakati fulani kulisababisha serikali ifikie uamuzi wa kuyapiga marufuku magari madogo aina ya Coaster ambayo miaka kadha huko nyuma yalikuwa maarufu kwa kubeba abiria kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Kwa upande mwingine wingi wa ajali katika eneo hilo, ulikuwa ni moja ya vyanzo vikuu kabisa vya kuufanya mkoa huo kuwa na askari wengi wa barabarani kuliko ilivyo katika maeneo mengine nchini.

Askari hao wamekuwa wakijulikana kwa namna wanavyokagua magari katika maeneo mbalimbali ya barabarani ya mkoa huo na hususan katika mji wa Kibaha ambao ndiyo yalipo makao makuu ya Mkoa wa Pwani.

Kwa bahati mbaya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na asasi za umma na hata kelele dhidi ya madereva wa magari ya abiria kuhusu haja ya wao kuwa makini wakati wanapoendesha magari yao zinaonekana kugonga mwamba, hasa unapoyaangalia matukio ya hivi karibuni.

Tumelazimika kulikumbusha jeshi hilo kuongeza juhudi katika kazi hiyo ya uhakiki wa magari kutokana na kuendelea kutokea kwa ajali ya magari katika maeneo mbalimbali nchini.

Ajali zilizotokea hivi karibuni na kupoteza maisha ya watu kadhaa huku wengine wakiachwa na ulemavu wa maisha ni ushahidi kwamba, ajali bado ni tatizo ambalo, linapaswa kufanyiwa kazi zaidi, si na polisi pekee, bali pia na wadau wengine mbalimbali wanaotumia barabara.


Tanzania Daima


 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 

Mtumie Rafiki

 Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2007 Darhotwire.com All rights reserved.Design by Infocomtechnologies Limited.