Tafuta DHWTangazaTuandikie
Wizi wa Michuma waweza kudhibitiwa.

Wizi mkubwa unaoendelea wa vifaa vya magari na magari yenyewe unatokana na kuwepo kwa maduka mengi yanayouza bidhaa chakavu za magari maarufu kama skrepa.

Bidhaa hizi chakavu ambazo nyingi hugeuzwa spea ndio hasa
chimbuko la kuwepo kwa wizi mkubwa wa michuma na vifaa vyake.

Ili kuthibiti hali hiyo ningeshauri maduka yanayouza spea za magari au maskrepa kuwahoji watu wanaowauzia vifaa hivyo na kutoa taarifa Jeshi la Polisi ili kuweka uhalali wa bidhaa zilizopo katika maduka yao.

Kama wenye maduka hao wakiamua kufanya biashara halali ni
dhahiri kuwa mfumo wa kutoa taarifa polisi baada ya kuletewa skrepa utasaidia kuzuia wizi holela unaoendelea kila kukicha.

Ni kweli kuwa matukio ya hivi karibuni yaliyokwisha tokea
yanaonyesha wezi hao wa magari wana soko kubwa ndio maana
wanafanya kila juhudi kufanikisha wizi kwa kuteka magari au hata kuyaiba toka mahali yalipoegeshwa ili kupata mshiko wa fastafasta.

Kwa kuwa siku hizi kuna maduka mengi ambayo yanauza skrepa za magari ama spea kutoka katika magari ambayo yamepata ajali ,hivyo inawezekana hata magari yanayoibwa yakawa yanabadilishwa ili kufanikisha biashara hiyo haramu.

Maduka hayo huenda yakawa yanauza vifaa vya magari ambavyo
inawezekana yameibwa na watu wanaofahamu maduka ya kuuzia
skrepa ama spea za magari .

Huenda pia uroho na uchoyo wa wauzaji wa maduka hayo unaofanya wimbi la wizi kuwa kubwa zaidi. Kwani wakati mwingine naamini kuwa watu hawa wa madukani wanawafahamu wahusika wa wizi wa magari lakini wanawalinda kutokana na maslahi wanayoyapata baada ya kuiba na kuwapelekea kwenye maduka yao ili waweze kuviuza .

Hata polisi wanapoona kuwa wizi wa namna hii inafaa sana
kuwabana wenye maduka kwani wanajua nani anawauzia skrepa na zimetoka wapi. Kwani kwa kukabiliana na wauzaji wa spea za magari au skrepa polisi wanaweza kuwapata wezi wanaowapelekea vifaa hivyo na hivyo kuvunja genge la wezi wa magari .

Naamini kuwa kama mwenye duka atamhoji mtu anayemletea vifaa hivyo na kumpa maneno ya ubabaishaji kisha mmiliki wa duka hilo au mhusika anayeuza dukani hapo akatoa taarifa katika Jeshi la Polisi ili mhusika au wahusika wahojiwe, atakuwa amefanikisha kuzima mtandao huo wa wezi.

Lakini ikiwa mmiliki wa duka au muuzaji akinyamaza kimya hali akijua wezi wa magari ndio wahusika kwa kuendelea kununua spea za magari ya wizi atakuwa akiwaruhusu wezi hao kuzidi kuharibu amani na mali za watu.

Pia majirani mitaani wakitoa taarifa juu ya mienendo ya watu mtaani ambao wakati mwingine huwa na magari na kutokuwa nayo katika spidi ya udalali wakati wao si madalali na wala si wenye maduka ya magari.

Naamini kutilia shaka mwenendo wa mtu kutasaidia pia kupata undani wake na mnyororo mzima wa upataikanaji wa magari yake, huenda akawa dalali wa mali ya wizi kwani mazingira hayaonyeshi kuwa na uhalali katika spidi hiyo.

Kimsingi naamini kuwa siri ya mwisho ya kuzuia wizi huu wa magari ni kwa wamiliki wa maduka ya spea na skrepa kuhoji watu wanaokwenda kuwauzia vifaa vya magari katika maduka yao na taarifa hizi kufikisha polisi ama kwa uwazi au kwa usiri .

Habarileo.









 Gonga hapa kutoa maoni yako kuhusu story hii...!!!
 Gonga hapa kusoma maoni hayo...!!!

 

Mtumie Rafiki

 Print nakala

 

Archive/Kumbukumbu:


Copyright © 2008 Darhotwire.com All rights reserved.Design by Infocomtechnologies Limited.