Si wakati wa kuendekeza Uswahiba.
Serikali imeonywa kutowachagua wenyeviti na wakurugenzi wa bodi za mashirika ya umma kwa misingi ya uswahiba, kulipa fadhila, dini na kabila, bali ifanye hivyo kulingana na uwezo wa wahusika hao.
Baadhi ya wabunge, watendaji na wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma walipokuwa kwenye kikao cha wabunge wa kamati ya hesabu za mashirika ya umma, wenyeviti na watendaji wakuu wa mashirika ya umma.
Ni wakati muafaka sasa baada ya Rais Jakaya kuwapa madaraka marafiki zake wa karibu kwa nia nzuri tu lakini mastokeo waliboronga kumtia aibu kiongozi wetu huyo baada ya kuibuka ufisadi katika sehemu mbalimbali na kufanya wahusika kuachia ngazi.
Peter Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), alisema umefika wakati kwa Serikali kuangalia watu wa kuwapa nafasi ya kuendesha mashirika ya umma na kuachana tabia ya kutoa madaraka kwa watu wasiostahili.
Alisema watu wasiostahili wanapopewa madaraka huwa chanzo cha shirika au taasisi za serikali kutofanya vizuri, hali inayosababisha taifa kupata hasara kubwa pamoja na kupoteza ajira kwa baadhi ya watumishi.
Elisa Mollel, Mbunge wa (CCM) Arumeru Magharibi, alisema ufanisi katika mashirika hayo unategemea zaidi kuchagua kiongozi mwenye taaluma katika sekta husika pamoja na uzoefu alionao kwenye uongozi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, alisema ni vema watendaji wa mashirika na taasisi za serikali wakawa makini katika utiaji saini mikataba ili kuepuka mambo ya ufisadi ambayo yameligharimu taifa fedha nyingi.
Alisema kila kukicha taarifa za ufisadi ndizo zinazopewa nafasi katika vyombo vya habari na watendaji wamekuwa wakitumia muda mwingi kushughulika na mambo hayo, jambo linalofanya muda wa kushughulikia maendeleo kuwa mdogo.
“Muda mwingi tunautumia katika kupiga kelele kuhusu ufisadi, sasa ni wakati kwa wenzetu kufanya kazi kwa umakini ili tuweze kwenda mbele na kutimiza malengo yetu,” alisema Zitto.
Source Tanzania Daima.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki
Print nakala